Hizo Posho za Simba, Yanga kasheshe TUPU

Monday June 1 2020

 

By OLIPA ASSA

STRAIKA wa Polisi Tanzania, Matheo Anthony amesema kucheza ndani ya timu hiyo kumemfumbua macho kuona fursa ya kufika mbali katika kazi hiyo.

Alifunguka kuwa wakati anacheza Yanga alikuwa anaona akiondoka maisha yake yangeweza kuwa magumu na pengine kukosa taswira,baada ya kuondoka akaona mawazo yake yalikuwa potofu.

“Ujue Simba na Yanga ni klabu ambazo posho zake zinaweza zikawa zinamchanganya mchezaji asiwaze mbali ya pale, kumbe wakati mwingine unaweza ukawa unaua kipaji chako kama hupati nafasi.

“Naamini nikujituma naweza kwenda nje kuvuna pesa kuliko zile posho ambazo zilikuwa zinanijengea hofu ya kwenda kucheza timu ambayo nitapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza,” alisema.

Alisema baada ya kuanza kucheza kikosi cha kwanza Polisi Tanzania anaona anaweza akafanya mengi ambayo hata Yanga yenye inaweza ikamrejesha ndani ya kikosi.

“Hakuna timu ambayo inaweza kumuacha ama isimpange mchezaji mwenye kiwango cha juu,hivyo napigania kuwa kwenye ubora mkubwa utakaofanya soko ama biashara yangu ya soka iwe vizuri,” alisema.

Advertisement

Hoja yake imeungwa na Yusufu Mhilu wa Kagera Sugar ambaye anamiliki mabao tisa kwamba kiwango cha mchezaji ndicho kitakachompa thamani.

“Simba na Yanga zinahitaji wachezaji wenye viwango,hivyo kama unataka kuzichezea lazima uonyeshe uwezo wa juu, binafsi baada ya kuondoka Jangwani sasa ninafunga kwa sababu napata nafasi,” alisema.

Advertisement