Fabinho apiga debe Mbappe atue Anfield

Tuesday January 14 2020

 

LIVERPOOL, ENGLAND. SI unajua Fabinho na Kylian Mbappe walikuwa wote AS Monaco na waliupiga mwingi sana kubeba ubingwa wa Ufaransa mwaka 2018?

Basi buana, baada ya kila mmoja kuchukua njia zake, Fabinho akitua Liverpool na Mbappe akienda zake Paris Saint-Germain, sasa wawili hao wanashawishiana waungane tena kwenye timu moja.

Na kinachotokea ni huyu Mbrazili wa Jurgen Klopp, Fabinho kupiga ndogondogo kumshawishi Mbappe aende wakaungane pamoja huko Anfield ili wawanyooshe wapinzani.

Hata hivyo, kumshawishi Mbappe atue Liverpool itakuwa shughuli pevu kwani fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa anaripotiwa kuwa kwenye rada za Real Madrid, lakini dau lake analouzwa si la kitoto. Kinachoelezwa ni kwamba PSG wanataka walipwe Pauni 257 milioni ili kuachana na staa wao huyo. Je, Liverpool wanayo pesa hiyo?

Mbappe na Fabinho walipocheza pamoja Monaco walishinda Ligue 1 msimu wa 2017-18 wakiwa chini ya kocha Leonardo Jardim huku wakiitoa pia Manchester City kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Fabinho aliulizwa anadhani ni mchezaji gani atashinda Ballon d’Or hapo baadaye, ndipo alipomtaja Mbappe na kumwomba aende akaungane naye Anfield.

Advertisement

Fabinho alisema: “Mbappe atashinda Ballon d’Or kabla ya Neymar. Ningependa kumkaribisha Liverpool.”

Mbappe amefunga mabao 11 kwenye Ligue 1 msimu huu huku akiiweka kwenye nafasi nzuri ya kubeba ubingwa huo wa Ufaransa kwa msimu mwingine mfululizo akiwa na wababe PSG.

Advertisement