Etienne: Majukumu yote Stars, Azam nayamudu

Muktasari:

Ndayiragije  msimu uliopifa alionyesha ubora wake kwa kuiongoza KMC ambayo ilikuwa imepanda daraja baada ya kujiunga nayo akitokea  Mbao FC ya Mwanza na kuifanya imalize nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzanuia Bara.

KATI ya vitu ambavyo kocha Etienne Ndayiragije amesema havimuumizi kichwa ni kumudu kuiongoza Azam huku akiwa na kibarua kingine cha kukaimu nafasi ya ukocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘ Taifa Stars’.
Ndayiragije tangu atimuliwe Emmanuel Amuneke baada ya kufanya vibaya kwenye Fainali za mataifa ya Afrika   ‘AFCON’ nchini Misri alipewa nafasi hiyo na Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Ndayiragije  alisema anapokuwa na majukumu ya kuiongoza Azam  huwa anatimiza majukumu yake kwa asilimia  zote  na pindi ambapo anaiongoza Stars anabadilika  na kuwa  mtu mwingine kimajukumu.
“Muda ambao kunakuwa na michezo ya timu ya Taifa programu zote za klabu husimama ni kipindi  ambacho nilikuwa nakitumia kupumzika lakini kwa sasa nimekuwa nikiingia kwenye majukumu mengine ya kuiongoza Stars kwa kushirikiana na wenzangu,” amesema.
Ameendelea kusema tabia ya kuwa makini kufuatilia kila kinachoendelea kwenye Ligi hata kama hakimuhusu kwa maana ya michezo imekuwa faida kwake akiwa na majukumu ya Taifa Stars ambapo hujua wachezaji walio kwenye viwango bora.
 “Tunafanya kazi kwa ukaribu na wenzagu ndio maana imekuwa rahisi kufanya uchaguzi wa wachezaji,” anasema kocha huyo ambaye ni raia wa Burundi.
Akizungumzia  maandalizi ya  kikosi chake za  Azam kuelekea mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya  Triangle United ya Zimbabwe , keshokutwa  Jumapili  uwanja wa Chamaz alisema yanaendelea vizuri na anaimani wataibuka na ushindi.
“Kila kitu kinaenda kama ambavyo tumepanga kwa kiasi kikubwa kilichobaki ni kukukifanyia kazi kile tulichokuwa tukijiandaa nacho. Kikubwa ni ushindi ndicho tunachokihitaji ili tuwe na mwanzo mzuri,” alisema kocha huyo.