MEZA YA UFUNDI : Dhana ya dawa za kuongeza nguvu haijawasaidia wachezaji

Saturday November 3 2018Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu jkanakamfumu@gmail.com

KWA muda mrefu wachezaji wa kitanzania wamekuwa na kasumba ya kutumia kilevi aina ya bangi wakidhani kuwa si sehemu ya dawa zinazokatazwa,

wamekuwa wakichukulia uvutaji wa bangi kwenye soka na michezo mingineyo kama ujana flani na sifa kwa mchezaji anayetuma.

Wengi wamechukua dhana ya uvutaji wa bangi kama kileo kinachowafanya kujituma uwanjani na wengine kuamini bila kuvuta hawawezi kucheza eti miili inakufa ganzi hivyo lazima kuwepo na ‘Stimu’.

Hali hii imedumu kwenye soka kwa muda mrefu, wachezaji wa zamani toka enzi hizo wamekuwa wakitumia kilevi hicho bila kificho si viongozi wala kocha ambao wamekuwa mstari wa mbele kukemea, kila mtu amekuwa akiona ni sawa tu vijana waendelee. Matumizi haya yamekuwa yakirithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na hakuna mchezaji anayeweza kukataa kuwa hatumii kilevi hicho au haoni wenzake wakitumia, bado imeonekana ni jambo la kawaida.

Wachezaji wamejenga dhana kuwa matumizi ya kilevi hicho hayahusiani na matumizi mengine ya vilevi vinavyokwenda kuongeza nguvu mwilini, husahau Mataifa yaliyoendelea wanamichezo hupimwa kutokana na matumizi ya dawa zile zinazotengenezwa viwandani, lakini dhana kubwa iliyojengeka miongoni mwa wachezaji ni kuwa matumizi yadawa hizo huwafanya wapate hamu zaidi ya kula chakula kingi kinachowasaidia kuongeza nguvu mwilini.

Kwa hapa Tanzania hali hiyoimesambaa kama nilivyosema kuwa imekuwa ikihama kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na imeenea kwenye kila eneo la michezo imeenea sasa hata kwenye taasisi na makundi ya michezo si soka tu. Chunguza kwa undani lazima kwenye wachezaji kumi utawakuta wanne wanatumia kileo hicho.

Lakini tatizo hili limeenea miongoni mwa wachezaji kwa sababu hakuna mtu anayewatuhumu na kuwakatalia wasifanye hivyo, hakuna taasisi yoyote nchini iliyowahi kuundwa ili kupinga matumizi ya kilevi hicho kwenye soka wala sijawahi kusikia msisitizo wa dhati kutoka kwa viongozi wa timu husika au uongozi mkubwa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na hata wakitoa matamko ufuatiliaji unakuwa mbovu.

Iwapo RADO wangeweza kufanya shitukizo la upimaji kwa wachezaji wetu bila shaka pasipo wasi timu zingelazimika kufanya usajili upya wa dharula kwa sababu si rahisi kuona timu nzima ikikosa watumiaji wa kileo hiki. Hali hii inaonekana ikipata sapoti ya baadhi ya viongozi wa klabu husika, kama siyo Katibu Mkuu basi unaweza kumkuta mtunza vifaa anahusika kwenye.

Lakini kwa ujumla wake matumizi ya kilevi hiki kiufundi hayajawahi kuwasaida wachezaji wetu zaidi ya kuwafanya wawe ni wenye kupata maonyo kila mara, matumizi haya ni kama yale matumizi ya nguvu za giza au matumizi ya miti shamba na Kamati nyingi zinazoitwa za ufundi nje ya Kocha Mkuu, matumizi haya kwa Watanzania na mifano tunayo ambapo baadhi ya wachezaji wanaodhaniwa kuwa wanatumia kilevi hicho wamekuwa wakifanya vitendo vingi vya ukiukwaji wanidhamu kila mara.

Matumizi ya dawa za kuongezanguvu ya aina hayajaisaidia nchi wala wachezaji wenyewe zaidi ya kuwafanya kuporomoka viwango vyao na kuharibu hata maisha yao ambayo yangewasaidia kupata timu nje ya nchi.

Wengine walishindwa kuvumilia kuishi mbali na makazi yao yaliyowazoesha kuwapa vitu hivyo na bila shaka mwanzo wa kutopata wachezaji wengi wanaocheza nje, wapo waliowahi kwenda nje na wakarudi wakiofia kupimwa au wakiofia kutopata dawa hivyo wakidhani itawapunguzia uwezo wakufanya vizuri uwanjani.

Matumizi ya kilevi hicho yamekuwa na athari kubwa kwa wachezaji ambapo makocha wamekuwa wakipata taabu kufikisha mafunzo yao salama kwa wachezaji.

Makocha wamekuwa wakipata taabu pale wachezaji wawapo ndani ya michezo na kisha kuwapa ujumbe ambao huwa hautekelezwi kwa asilimia zote, mara nyingi walimu hushindwa kuelewa kwa nini yale wanayoyafundisha hayatimizwi na bila shaka matokeo yake huwa si salama na ndiyo moja kati ya sababu zinazopelekea timu na wachezaji wetu kushindwa kufanya vizuri.

Viongozi wanapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa wachezaji wetu kwani itasaidia kubeba taifa letu kwenye michezo hasa tunapopata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa na hapo ndio utakua mwanzo kwa vijana wetu kuonyesha uwezo wao kwa timu za nje kwa kujitangaza wanapofanya vizuri.

Hakuna maendeleo ya mchezaji yanayokuja kwa kuota au kudanganywa na kufanya vitu visivyo na maadili, kujituma na nidhamu ya mchezaji ni moja ya vitu vinavyoangaliwa kwa mchezaji anapotakiwa kusajiliwa.

Ni wajibu wetu kuelimisha na kukoleza elimu ya kutotumia tena kilevi hicho michezoni.

Advertisement