‘Basketball Africa League’, pishi jipya la Amadou Gallo Fall

Muktasari:

Amadou alikuwa anawaza kuwa dunia nzima inatamani kuingia kwenye NBA, bahati mbaya wachezaji 450 tu ndio wanaoweza kuwepo katika timu 30 za NBA kila mwaka.

Wiki iliyopita nilisafiri zaidi ya maili elfu sita kutoka Dar es Salaam mpaka Senegal kuja kushuhudia rekodi ikiandikwa, rekodi ya mabadiliko katika sekta ya michezo.

Ndoto mpya ilikuwa inazaliwa na kulikuwa na mwanga unaomulika baada ya muda mrefu kuishi katika giza totoro ambalo tulikuwa tunajitahidi kutazama na hata tusione mbali.

Nchini Senegal, kwenye jiji la Dakar kulikuwa kuna Simba mmoja aliyekuwa anatoka kuwa Simba wa Teranga na kwenda kuwa Simba Mfalme wa Afrika. Anaitwa Amadou Gallo Fall ambaye anafahamika kuwa Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), lakini pia akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa NBA Afrika. Baada ya kupambana kwa miaka zaidi ya ishirini, akishuhudia mikono yake ikipeleka vijana wengi wa Afrika kucheza NBA, kwenye medula ya Amadou Gallo kulikuwa na picha tofauti zaidi.

Amadou alikuwa anawaza kuwa dunia nzima inatamani kuingia kwenye NBA, bahati mbaya wachezaji 450 tu ndio wanaoweza kuwepo katika timu 30 za NBA kila mwaka. Nchi ya Marekani peke yake ina vijana zaidi ya laki moja kila mwaka wenye ndoto ya kuingia NBA kabla hujawaza mataifa ya Ulaya.

Safari yake mpya ya kujenga mpira wa kikapu ikaanza baada ya kuwepo kwa ‘project’ maarufu inayoitwa SEED PROJECT. Akiishi ndoto zake akasimamia programu za kusaka vipaji za Basketball Without Boarders, ambapo wakazaliwa akina Luc Mbah Moute, Gorgui Dieng, mpaka leo hii Joel Embiid na bingwa wa NBA Pascal Siakam. Ikiwa imesimama akaondoka zake Marekani na kurudi kuanzisha ofisi za NBA barani Afrika, akafungua programu za vijana kama NBA Academy Afrika na JR NBA ambayo ipo mpaka Tanzania.

Miaka takribani tisa baadaye amekuja na ukombozi rasmi wa wachezaji wa mpira wa kikapu wenye ndoto. Amadou Gallo akishirikiana na NBA wanaanzisha kile kilichokuwa kinaonekana kuwa mtihani na kisichowezekana, Ligi Maalumu ya Afrika ya Mpira wa Kikapu itakayosimamiwa na NBA na FIBA.

Amadou Gallo atakuwa rais wa ligi hii mpya itakayofahamika kama ‘BASKETBALL AFRICA LEAGUE’ (BAL) ambayo imekuwa ndoto iliyogeuka kuwa kweli. Mfumo wa ligi hiyo utahusisha timu 12 kwa kuanzia lakini itaendelea kutanuka kuendana na miundombinu inavyokua. Mataifa ya Senegal, Tunisia, Angola, Morocco, Misri na Rwanda yatahusika kwenye kuandaa huku Rwanda ikipewa heshima zaidi kuandaa nusu fainali na fainali.

Chapa za Nike na Jordan ndio zitakazohusika kwenye uzalishaji wa jezi rasmi za mashindano haya na kikubwa zaidi ni mkakati uliowekwa na NBA kwenda mbali zaidi kuhakikisha kuwa kila nchi inapata ushiriki ndani ya miaka michache ijayo.

NBA wamepanga kushiriki mikutano mikuu ijayo ya Umoja wa Mataifa (UN) na watakuwa wanaweka mezani hoja za maendeleo ya michezo hususani mpira wa kikapu Afrika.

Ndoto pekee ni kuwa na viwanja na miundombinu iliyowezekana Kigali na Dakar kwenye majiji mengine kama Dar es Salaam, Nairobi, Kampala mpaka Kinshasa. ‘Basketball Africa League’ inakuja si tu kubadili uhalisia wa mchezo huu bali pia kutoa fursa mbalimbali. Elimu, stadi za maisha, teknolojia, afya na ujasiriamali hususani kwa vijana ni ajenda za Amadou, BAL ikiwa ni kuhakikisha shule, taasisi za elimu kama vyuo, wawekezaji, Serikali na wadau wote wanasimamia nafasi zao katika kuelekeza vijana katika njia sahihi.

Amadou kwa sasa anapika chakula, chakula chenye ladha ya kipekee, chakula kitamu, kinachovutia na chenye harufu isiyomithilika. BAL ni lishe kwa vijana wengi, lishe inayoandaliwa na mpishi maridadi na mwenye nia ya kila kijana mwenye ndoto kujing’ata vidole vyao kwa utamu.

Chakula ambacho kimemvutia mpaka Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama na amenukuliwa akisema atataka kuwa sehemu ya watakaokigawa kwa walaji kwa maana ya kuwa sehemu ya uwekezaji.

Wakati uwanja wetu wa Ndani wa Taifa ukiwa katika hali mbaya, nyakati kama hizi ndizo ambazo zinatupasa kutoka kwenye usingizi wa pono, zinatupasa kutucharaza viboko ili sisi punda tusogeze mzigo ufike. Lazima tukubali walau kukimbia wakati wenzetu wameshagundua usafiri wa kuwafikisha kwenye sayari ya ndoto yao.

Afrika ni sasa ndio imekuwa kampeni ya kipindi kirefu lakini Amadou ameileta kwenye uhalisia na sasa tunaiona. Huyu anabaki kuwa mtu muhimu zaidi kwenye michezo Afrika kwa sasa na anayehitaji sapoti kwa sababu ameshikilia ndoto ya maelfu ya Watoto wa Afrika kwa miaka kenda na zaidi ijayo. Tumkumbatie, tumpe nafasi, tumwamini na tumsaidie kwa sababu ameamini na ameweka kwenye uhalisia mfupa uliowashinda wengi.