Barca yakomaa kumnasa De Ligt

BARCELONA HISPANIA. BARCELONA imegoma kukata tamaa na hivyo itakomaa mwanzo mwisho kwenye mpango wao wa kunasa saini ya beki wa kati wa Juventus, Matthijs de Ligt.

Miamba hiyo ya Hispania, sambamba na Manchester United, kwa muda mrefu wamekuwa wakimfukuzia Mdachi huyo tangu kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, lakini Juventus ilishinda kwenye mbio hizo za kunasa huduma yake akitokea Ajax.

De Ligt amecheza mechi 27 tu Juventus msimu huu, lakini kiwango chake kimezua maswali na sasa staa huyo anaweza kufunguliwa mlango mwishoni msimu ujao.

Barca waliripotiwa kuweka mezani Pauni 66 milioni kunasa saini ya beki huyo mwaka jana, lakini Juventus iligomea ofa hiyo, na sasa miamba hiyo ya Nou Camp inapambana kuhakikisha wanamnasa Mdachi huyo.

Kikosi hicho cha Quique Setien kimeripotiwa kwamba, kitaingia sokoni kusaka beki wa kati mpya kuwapa changamoto Clement Lenglet na Gerard Pique, huku Samuel Umtiti akidaiwa kwamba atafunguliwa mlango wa kutokea.

Real Madrid nayo ipo vitani kuisaka saini ya De Ligt, licha ya kusaini mkataba wa miaka mitano wakati alipotua Juventus Julai mwaka jana.

Man United baada ya kukosa huduma yake mwaka jana ilikwenda Leicester City kumsajili beki Harry Maguire na kuweka rekodi ya kumfanya awe beki ghali zaidi duniani kwa sasa, ilipomnasa kwa Pauni 85 milioni.

Hata hivyo, kama Juventus wakitangaza kupokea ofa kwa ajili ya huduma ya beki huyo, basi Barcelona na Real Madrid zinaweza kupambana kumwania kutokana na wote kuwa na mahitaji naye ili kumfanya kuwa mbadala wa mabeki wao wa kati ambao, wameanza kuchoka.