Barbara: Nina makocha wapya watatu

MAKIPA wa timu ya Simba wanaendelea kujifua bila ya kuwa na kocha wao, Mharami Mohammed ‘Shilton’ aliyetimuliwa sambamba na meneja Patrick Rweyemamu, siku chache tangu timu hiyo ilipopoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting.

Mabosi wao wapo bize kusaka kocha mmoja mkali wa kuziba nafasi hiyo ili kuendelea kuwaweka kwenye viwango bora na tayari wamesaliwa na majina matatu kati ya matano ya walioomba kazi klabu.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aliliambia Mwanaspoti kuwa, kocha mpya wa makipa anatarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia leo, kwani mchakato wa kupitia wasifu wa makocha walioomba kazi umefikia pazuri.

Shilton alitemwa na Rweyemamu kwa kilichoelezwa kutokuwa na maelewano mazuri na kipa Beno Kakolanya, huku pia akidaiwa kushindwa kutatua makosa yanayojirudia kwa makipa wake, Aishi Manula na Beno kufungwa mabao ya aina moja kila mara. Kabla ya kuwa kocha wa makipa, Shilton aliyefananishwa na kipa wa zamani wa England, Peter Shilton, aliwahi kuidakia timu hiyo pamoja na Taifa Stars kabla ya kucheza soka la kulipwa nchini Msumbiji.

Juu ya mtu wa kuziba nafasi yake, Barbara alisema kuna makocha watano waliomba nafasi hiyo na wapo kwenye hatua nzuri kumpa mmojawao.

“Tulikuwa na majina matano ya walioomba nafasi ya kuchukua nafasi ya kocha wa makipa, lakini tumesaliwa na watatu ambayo tunaendelea kuyajadili kabla ya kumtangaza mmoja wao baada ya kukubaliana naye,” alisema Barbara aliyekataa hata hivyo kutaja majina ya makocha hao.

“Ni vigumu kuweza kutaja majina yao wakati hatujamalizana nao, pia wengine ni waajiriwa kwenye klabu nyingine, hivyo tukitangaza kabla ya kumalizana nao tunaweza kuwaharibia, ila kila kitu kipo vizuri kwa upande huo,” alisisitiza. Miongoni mwa majina hayo matatu, limo pia jina la kocha wa makipa wa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Crannes’, Fred Kajoba ambaye pia anaifundisha Vipers iliyoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Simba imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi.

Barbara aliyefichua tangu ameingia kama mtendaji mkuu amekuwa akirekebisha baadhi ya mambo ndani ya klabu hiyo hasa kwa watumishi.

Alisema kwa sasa wameweka utaratibu wa kila mtumishi kuwa na mwongozo wa utendaji kazi kuanzia kwa makocha mpaka watumishi wengine, akieleza kabla ya hapo jambo hilo halikuwepo ndio maana baadhi yao wameamua kuachana nao hivi karibuni.

“Huu ni utaratibu wa kazi kokote, nasi tumeona tuufanye ndani ya Simba kwa sababu ya kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Barbara aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia cheo hicho kwenye upande wa soka kwa ngazi za klabu nchini.