Zizou, Beckham ndani ya tangazo Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Nyota wa Barcelona, Lamine Yamal na supastaa wa Real Madrid, Jude Bellingham, wanaweka pembeni uhasama wa El Clasico na kuungana katika timu moja, huku nyota wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani, Trinity Rodman akikamilisha kikosi hicho.
WASHINGTON, MAREKANI: ADIDAS wameingia Hollywood baada ya kuzindua tangazo la thamani ya zaidi ya Pauni 50 milioni kwa ajili ya Kombe la Dunia litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11, mwaka huu.
Tangazo hilo la dakika tano limejaa mastaa wa soka na filamu kiasi cha kuonekana kama filamu kamili ya Hollywood, likimuonyesha muigizaji maarufu Timothee Chalamet ndiye mhusika mkuu akikusanya timu ya ndoto ya watu watatu kwenda kupambana na mabingwa wa mtaani ambao hawajafungwa kwa miaka 30.
Nyota wa Barcelona, Lamine Yamal na supastaa wa Real Madrid, Jude Bellingham, wanaweka pembeni uhasama wa El Clasico na kuungana katika timu moja, huku nyota wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani, Trinity Rodman akikamilisha kikosi hicho.
Katika simulizi hiyo, Chalamet anasimulia namna timu hiyo ya mtaani ilivyowahi kuwafunga mastaa wakubwa wa dunia wakiwamo Zinedine Zidane, David Beckham na Alessandro Del Piero, huku Lionel Messi pamoja na mwanamuziki Bad Bunny wakionekana pembeni wakitazama mchezo huo kwa utulivu.
Tangazo hilo pia limewahusisha mastaa wengine kama Ousmane Dembele, Raphinha, Pedri, Florian Wirtz na Santiago Gimenez. Chalamet amesema ana uhusiano wa karibu na viwanja vya Pier 40 mjini New York ambako sehemu kubwa ya tangazo hilo ilirekodiwa.
“Niliwahi kuota kucheza na mastaa hawa. Nilikuwa nikicheza Pier 40 nikiwa mtoto nikijaribu kuiga free-kick za Beckham, mabao ya Del Piero na ukokotaji mpira wa Zidane. Ninalipenda sana boli, hivyo kufanya kazi hii na Adidas pamoja na mastaa hawa ni jambo kubwa sana kwangu,” amesema. Wataalamu wa matangazo wanaamini Adidas walitumia zaidi ya Pauni 50 milioni kulitengeneza na kwamba Messi, Beckham na Zidane inaaminika wamelipwa mamilioni ya pauni kuonekana. Teknolojia ya kisasa ya AI pia imetumika kumuonyesha Beckham akiwa na mitindo mbalimbali ya nywele aliyowahi kuwa nayo katika maisha yake ya soka.