Familia ya Beckam ngoma bado ngumu
Muktasari:
- Brooklyn ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wanne wa David na Victoria Beckham, alitoa tamko la kushtua katika mitandao ya kijamii akiwashambulia wazazi wake, familia yao na jinsi walivyomtendea mke wake, Nicola Peltz Beckham.
INAELEZWA bado familia ya nyota wa zamani wa Manchester United, David Beckham iko kwenye mgogoro mkubwa na mtoto wao Brooklyn Beckham.
Brooklyn ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wanne wa David na Victoria Beckham, alitoa tamko la kushtua katika mitandao ya kijamii akiwashambulia wazazi wake, familia yao na jinsi walivyomtendea mke wake, Nicola Peltz Beckham.
Hata hivyo, Beckham na mkewe wamekuwa wakimsihi mwanao huyo kuachana na mambo hayo na kusamehe ili kurejesha uhusiano wao uliovunjika, wakihofia kutengwa na maisha ya wajukuu zao wa baadaye.
Mgogoro huo ulianza Januari 2026, baada ya Brooklyn, 27, kutoa kauli hadharani akiwashutumu wazazi wake kwa kuendesha maisha ya familia kwa maonyesho ya mitandao ya kijamii lakini kiuhalisia wa ndani wakiigiza tu.
Brooklyn na mke wake, Nicola Peltz Beckham wanaripotiwa wanataka kuanzisha familia hivi karibuni, jambo ambalo limeongeza hofu kwa David na Victoria kutafuta suluhisho haraka ili kuwa karibu na wajukuu zao. Victoria anaripotiwa kuumia na wazo la kusikia habari za mjukuu kupitia vyombo vya habari badala ya kumpokea kwa mtoto wake mwenyewe.
Mgogoro huo ulianza hata kabla ya harusi ya Brooklyn mwaka 2022, lakini hali ilizidi kuwa mbaya mwaka huu baada ya Brooklyn kudai wazazi wake walijaribu kuharibu ndoa yake na kusambaza taarifa zisizo sahihi kwenye vyombo vya habari.
Amesema wazi hana nia ya kupatana nao kwa sasa na angependa kushughulika nao kupitia wanasheria tu. Kwa upande mwingine, David na Victoria inaelezwa wana hofu kama wazazi kumpoteza kijana wao mkubwa na kukosa kushiriki sehemu ya maisha ya watoto na wajukuu.
Beckham aliwahi kusema: “Nimejaribu kufanya vivyo hivyo kwa watoto wangu, kuwaelimisha. Wanafanya makosa, lakini watoto wanaruhusiwa kufanya makosa. Hivyo ndivyo wanavyojifunza.”
Nicola aliwahi kusema mwaka 2022 wanatamani kuwa na familia kubwa, ikiwemo kuzaa na kuasili watoto, huku Brooklyn naye akisema angependa kuwa na watoto wengi kama timu ya mpira wa miguu.
Baadhi ya mastaa wanatajwa kujaribu kusaidia kuwapatanisha familia hiyo ingawa hadi sasa juhudi hizo hazijazaa matunda.