Zidane ang'oka Real Madrid
Muktasari:
- Zinedine Zidane amejiuzulu kazi ya ukocha wa Real Madrid, kwa mujibu wa vyombo vya habari, baada ya kuvuliwa ubingwa wa soka wa Hispania na Atletico Madrid.
Madrid, Hispania (AFP). Zinedine Zidane amejiuzulu kazi ya ukocha wa Real Madrid, kwa mujibu wa vyombo vya habari, baada ya kuvuliwa ubingwa wa soka wa Hispania na Atletico Madrid.
Taarifa za kuondoka kwa Mfaransa huyo zimekuja mwishoni mwa kampeni iliyokuwa mbaya kwa vigogo hao ambao wametwaa ubingwa wa Ulaya mara 13, baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Chelsea katika nusu fainali na hivyo kumaliza msimu kwa mara ya kwanza katika miaka 11 bila ya kombe lolote.
Mwandishi wa soka wa Italia, Fabrizio Romano alitoa habari hiyo aliyoita ya kipekee katika akaunti yake ya Twitter na baadaye vyombo vya habari vya Madrid kuibeba, hasa magazeti ya Marca na AS, na kituo cha redio cha Cadena Ser.
Taarifa rasmi za kuondoka kwake zinatazamiwa kutangazwa wakati wowote.
Siku kumi tu zilizopita Zidane, ambaye ana mkataba hadi mwaka 2022, alikanusha taarifa kuwa ameshawaambia wachezaji wake kuwa anaondoka mwishoni mwa msimu.
"Ninawezaje kuwaambnia wachezaji wangu kuwa naondoka sasa? Ni uongo," alisema baada ya Real kuishinda Athletic Bilbao kwa bao 1-0.
"Naelekeza nguvu katika msimu huu. Kuna mechi imebakia lakini tutafanya kila tuwezalo. Nachoangalia ni kinachotokea mwishoni."
Lakini, pengine kwa kudokeza, aliongeza: "Mengine, tutaona mwishoni mwa msimu."
Kama ikithibitishwa, huo utakuwa mwisho wa enzi ya pili kwa Zidane katika timu hiyo.
Kiungo huyo aliyetwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa na Ufaransa alishika hatamu Januari 2016 na kuiongoza Real kutwaa ubingwa wa La Liga mwaka 2017 na baadaye ubingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo kabla ya kuondoka ghafla Mei 31, 2018.
Alirejea mwaka 2019, na kuiongoza tena Real kutwaa ubingwa wa Hispania mwaka 2020 na Super Cup.