Zaha akiuzwa tu Man U inalipwa

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER United inajiandaa kupokea mkwanja mrefu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kama supastaa winga Wilfried Zaha ataamua kuachana na Crystal Palace.

Zaha, 28, ameripotiwa hajioni kama ataendelea kubaki Selhurst Park zaidi na hivyo ameshawaambia mabosi wa timu hiyo anataka kwenda kukabiliana na changamoto mpya.

Mkataba wake umebakiza miaka miwili huku Arsenal na Tottenham Hotspur zikionekana kuwa na dhamira ya dhati ya kunasa saini yake.

Kama Palace watakubali kumuuza basi mkwanja wowote utakaotolewa, Man United itapokea asilimia 25 ya mgawo.

Man United ilimsajili Zaha kutoka Palace kwa ada ya Pauni 10.58 milioni mwaka 2013, lakini baada ya kushindwa kuonyesha makali Old Trafford, akatolewa kwa mkopo Cardiff na Palace, kabla ya kutua jumla Selhurst Park kwa ada ya Pauni 6 milioni mwaka 2015. Man United iliweka kipengele kwenye mkataba wa mauzo ya Zaha, kama atauzwa tena na Palace, basi wao watalipwa asilimia 25 ya pesa itakayotolewa.

Palace waliwashawishi Man United wafute kipengele hicho wakati walipomsajili Aaron Wan-Bissaka mwaka 2019, lakini mabosi wa Old Trafford waligoma na hivyo kumnasa beki huyo wa kulia kwa pesa nyingi, Pauni 50 milioni.