Young, mwanaye mambo yamegoma
Muktasari:
- Wawili hao wangeweka rekodi ya kuwa mara ya kwanza kwa baba kukutana na mwanaye kwenye mechi ya Kombe la FA, wakati Everton ilipokabiliana na Peterborough United uwanjani Goodison Park kwenye raundi ya tatu ya michuano hiyo.
LONDON, ENGLAND: ASHLEY na Tyler Young wamenyimwa fursa ya kutengeneza historia kwenye Kombe la FA kwa watu wa familia moja kukutana kwenye mechi, jana Alhamisi.
Wawili hao wangeweka rekodi ya kuwa mara ya kwanza kwa baba kukutana na mwanaye kwenye mechi ya Kombe la FA, wakati Everton ilipokabiliana na Peterborough United uwanjani Goodison Park kwenye raundi ya tatu ya michuano hiyo.
Wakati Young Sr akiingia kwenye dakika 73, Tyler aliendelea kubaki benchini tu.
Kocha wa Peterborough, Darren Ferguson baadaye alisisitiza kwamba alifanya uamuzi sahihi wa kutomchezesha kinda huyo, aliposema: “Ilikuwa ngumu sana kumwacha Tyler kwenye benchi, lakini nimefanya hivyo kwa manufaa ya timu yangu. Ningemwingiza Tyler kama tungekuwa nyuma kwa mabao 2-0, lakini kuwa nyuma 1-0, nilihitaji kuingiza washambuliaji. Nilijaribu kutafuta kitu kwa ajili ya manufaa kwa timu. Na kitu kingine, haikuwa mechi ya hisani.”
Baada ya mechi, Young Sr alionekana akimpoza mwanaye kwa kushindwa kuandika historia hiyo huku mashabiki wakiwashangilia.
Baadhi ya mashabiki hao walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kupongeza hilo, ambapo mmoja aliandika: “Safi sana.”
Mwingine alisema: “Hii ni nzuri sana.”
Shabiki wa tatu alisema: “Hii ni aibu kubwa kwa Darren Ferguson!”
Everton ilipata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi hiyo, shukrani kwa mabao ya Beto na Iliman Ndiaye.
Nahodha wa timu hiyo, Seamus Coleman na beki wa zamani, Leighton Baines waliisimamia timu hiyo baada ya kocha Sean Dyche kufutwa kazi saa tatu kabla ya kuanza kwa mchezo huo.