Yoro, Hojlund washtua Man United

Muktasari:
- Yoro na Hojlund waliumia katika mchezo dhidi ya Arsenal ambao ulikuwa ni wa pili kwa Yoro kucheza tangu alipojiunga Man United.
LOS ANGELES, MAREKANI: MCHEZAJI mpya wa Manchester United aliyesajiliwa katika dirisha hili akitokea Lille kwa ada ya Pauni 59 milioni, Leny Yoro atakaa nje kwa miezi mitatu kutokana na majeraha aliyoyapata, huku Rasmus Hojlund akikaa wiki sita.
Yoro na Hojlund waliumia katika mchezo dhidi ya Arsenal ambao ulikuwa ni wa pili kwa Yoro kucheza tangu alipojiunga Man United.
Baada kuumia katika mchezo huo uliopigwa jijini Los Angeles, Yoro mwenye umri wa miaka 18, alionekana akichechemea huku akitembea kwa magongo Jumatano alipokuwa akienda kupanda gari la Man United kutoka kambini na wachezaji wengine.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na Man United zinaeleza staa huyo amevunjika mfupa wa mguu.
Man United itamenyana na Manchester City katika mchezo wa Ngao ya Jamii uwanjani Wembley, Agosti 10 kabla ya kuanza kampeni ya Ligi Kuu England dhidi ya Fulham siku sita baadae na katika mechi zote hizo staa huyu hatokuwepo.
Taarifa rasmi juu ya hali ya staa huyo ilitolewa jana lakini kabla ya hapo kulikuwa na ripoti zilizoibuka baada ya kusambaa kwa picha zake akiwa anatembea zilizoeleza anaweza kukaa nje kwa mwezi mmoja au miwili.
Katika eneo ambalo Yoro anacheza, Ten Hag alikuwa kitegemea kumtumia Lisandro Martinez lakini itakuwa ngumu kwa sababu fundi huyo amechelewa kuanza mazoezi baada ya kupewa mapumziko kufuatia kuitumikia Argentina katika michuano ya Copa America.
Sasa mastaa ambao wanaweza kuziba pengo lake ni Harry Maguire, Jonny Evans na Victor Lindelof.
Hata hivyo, Man United bado inataka kusajili beki wa pili wa katika dirisha hili na inaangalia uwezekano wa kumsajili beki wa kati Bayern Munich, Matthijs de Ligt na beki wa Everton Jarrad Branthwaite.
Bado kunaweza kuwa na habari mbaya zaidi kwa United baada ya Rasmus Hojlund pia kutoka nje ya mchezo wa Arsenal katika kipindi cha kwanza na kile kinachoonekana kuwa jeraha la misuli ya paja.
Mbali ya Yoro, mchezaji mwingine aliyeumia katika mechi dhidi ya Arsenal alikuwa ni Hojlund lakini alionekana akitembea kwa uhuru Jumatano hali iliyoashiria hakuwa ameumia sana.
Wakiwa katika maandalizi ya msimu mwaka jana, Man United ilipata pigo la majeraha kama ilivyokuwa sasa na Kobbie Mainoo na Amad Diallo walipata majeraha yaliyowafanya wakae nje ya uwanja hadi Novemba na Desemba.