Xavi Simons nje msimu mzima, kukosa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Tottenham imethibitisha Simons amepata jeraha la goti na atalazimika kufanyiwa upasuaji katika wiki zijazo kabla ya kuanza programu ya kupona chini ya madaktari wa klabu hiyo.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Xavi Simons amevunjika moyo baada ya kuthibitika atakosa msimu uliosalia pamoja na nafasi ya kucheza Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi kutokana na jeraha baya la goti.
Tottenham imethibitisha Simons amepata jeraha la goti na atalazimika kufanyiwa upasuaji katika wiki zijazo kabla ya kuanza programu ya kupona chini ya madaktari wa klabu hiyo.
Simons alipata jeraha hilo dakika ya 58 katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers baada ya kugongana na beki Hugo Bueno, alionekana kushika goti lake la kulia.
Alijaribu kuendelea na mchezo lakini alianguka tena mbele ya madaktari wa timu na hatimaye alitolewa uwanjani kwa machela.
Simons amesema: “Wanasema maisha yanaweza kuwa magumu na leo nahisi hivyo. Msimu wangu umefikia mwisho ghafla na bado najaribu kuelewa kilichotokea.”
Ameongeza: “Kwa kweli nimevunjika moyo. Nilichotaka ni kupigania timu yangu lakini sasa nimepoteza nafasi hiyo pamoja na Kombe la Dunia.”
Kukosekana kwa Simons ni pigo jingine kwa Tottenham, ambao wanapambana kuepuka kushuka daraja. Simons pia anajiunga na orodha ya majeruhi wengine kama vile nahodha Cristian Romero na kiungo Mohammed Kudus ambao nao watakosekana katika michezo yote iliyosalia ya msimu.