William Saliba ashtua Arsenal
Muktasari:
- Beki huyo alilazimika kutolewa mapema katika mchezo wa Arsenal dhidi ya Liverpool mwishoni mwa wiki na kwa mujibu wa jarida la L'Equipe, Saliba sasa atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa kati ya wiki tatu hadi nne.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepata pigo lingine baada ya kugundua muda ambao beki wao William Saliba atakaa nje kutokana na jeraha lake la kifundo cha mguu.
Beki huyo alilazimika kutolewa mapema katika mchezo wa Arsenal dhidi ya Liverpool mwishoni mwa wiki na kwa mujibu wa jarida la L'Equipe, Saliba sasa atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa kati ya wiki tatu hadi nne.
Saliba hajaitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kwa sasa, pia anatarajiwa kukosa michezo kadhaa ijayo ya taifa hilo.
Kwa upande wa Arsenal, beki huyo wa kati anaweza kukosa michezo ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest, Manchester City na Newcastle, pamoja na ule wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Athletic Bilbao.
Kutokuwepo kwa Saliba bila shaka ni pigo kubwa kwa Arsenal, lakini mchezaji aliyesajiliwa katika majira haya ya kiangazi, Cristhian Mosquera sasa anaweza kupewa nafasi zaidi za kuonyesha ubora wake.
Mosquera, 21, aliyejiunga na Arsenal kutoka Valencia, alionyesha kiwango kizuri baada ya kuchukua nafasi ya Saliba katika mchezo dhidi ya Liverpool.
Mbali ya jeraha la Saliba, Arsenal pia ina changamoto ya majeraha kwa wachezaji wengine tegemeo wa kikosi chao cha kwanza.
Bukayo Saka hayupo kikosini kutokana na tatizo la msuli wa paja ambalo linaweza kumfanya akose michezo kadhaa pia Kai Havertz hayupo kutokana na jeraha la goti.
Ben White na Christian Norgaard nao wako nje kwa sababu ya majeraha.
Gabriel Jesus anakaribia kurejea kutoka kwenye jeraha la kiungo cha mkono wa mbele (anterior cruciate ligament) ambalo limekumweka nje tangu Januari, lakini mshambuliaji huyo hakujumuishwa kwenye kikosi cha Arsenal kitakachocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal itakutana na Forest Septemba 13 katika mchezo wao wa kwanza baada ya mapumziko ya wiki ya kimataifa.