Wijnaldum: Slot? Mtu kama Klopp

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mdachi, Slot amethibitishwa kuwa ndiye mrithi wa Klopp huko Anfield. Na sasa amekuwa na presha kubwa kutokana na ugumu wa kibarua hicho alichorithi kutoka kwa Mjerumani, Klopp ambaye alipata mafanikio makubwa na miamba hiyo ya Anfield.

LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa zamani wa Liverpool, Georginio Wijnaldum amemlinganisha Arne Slot na makocha Jurgen Klopp na Jose Mourinho, akiamini atapata mafanikio kwenye kikosi hicho cha Anfield baada ya kuteuliwa kuwa kocha mpya wa miamba hiyo.

Mdachi, Slot amethibitishwa kuwa ndiye mrithi wa Klopp huko Anfield. Na sasa amekuwa na presha kubwa kutokana na ugumu wa kibarua hicho alichorithi kutoka kwa Mjerumani, Klopp ambaye alipata mafanikio makubwa na miamba hiyo ya Anfield.

Akiwahi kufanya kazi na Slot huko kwao Uholanzi, Wijnaldum anaamini kocha huyo mpya wa Anfield ataendelea kuifanya Liverpool kuwa kwenye mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja.

Akizungumza na  Algemeen Dagblad, kiungo huyo wa zamani wa Liverpool alisema: “Nilifanya mazoezi Feyenoord kwa siku kadhaa mwanzoni mwa msimu uliopita na niliona jinsi Slot anavyofanya kazi. Anafanya kwa viwango vikubw asana, naamini atakwenda kuwa mkubwa sana.

“Namlinganisha na Klopp na Mourinho na ninachosema Slot yupo kwenye viwango hivyo. Sawa, anataka kwenye dunia yenye ushindani tofauti kabisa, hilo ndilo linaloonekana kuwa tatizo, lakini je hataweza kwenda kufanya alichofanya Feyenoord akifika Anfield?”

Mmoja wa wachezaji wenzake wa zamani Wijnaldum, ambaye ni Mdachi mwenzake, Virgil van Dijk yupo tayari kutoa sapoti kubwa kwa Slot katika kuhakikisha mambo yanakwenda kwenye kikosi hicho.

Van Dijk alisema: “Kuna nafasi kubwa ya kuwa vizuri. Nasubiri kwa hamu msimu ujao ufike. Mabadiliko ni kitu kinachotishia kidogo, lakini tunaamini tuna watu wenye uwezo mkubwa na hakika Slot atakuja na kitu tofauti kwenye kikosi.”

MECHI ZA LIVERPOOL KWENYE PRE-SEASON

-Julai 27 v Real Betis (Acrisure Stadium, Pittsburgh)

-Julai 31 v Arsenal (Lincoln Financial Field, Philadelphia)

-Agosti 3 v Man United (Williams - Brice Stadium, South Carolina)