West Ham United mambo magumu EPL
Muktasari:
- Kikosi hicho kinachonolewa na Nuno Espirito Santo sasa kinaangalia hatari ya kushuka daraja moja kwa moja huku mahasimu wao wakubwa Tottenham Hotspur wakihitaji ushindi dhidi ya Chelsea leo ili kuwazamisha rasmi.
LONDON, ENGLAND: WEST HAM United ipo wakati mgumu na kuna uwezekano mkubwa wakashuka daraja baada ya kupokea kichapo kingine kutoka kwa Newcastle United juzi katika mchezo ambao walipaswa kushinda kwa udi na uvumba.
Kikosi hicho kinachonolewa na Nuno Espirito Santo sasa kinaangalia hatari ya kushuka daraja moja kwa moja huku mahasimu wao wakubwa Tottenham Hotspur wakihitaji ushindi dhidi ya Chelsea leo ili kuwazamisha rasmi.
West Ham walionekana kurejea kwenye mstari baada ya ushindi mfululizo dhidi ya Wolves na Everton mwezi uliopita, lakini Newcastle waliwazidi kila kitu katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa St James’ Park.
Bao la kwanza lilitokana na uzembe mkubwa wa West Ham walipokuwa wakicheza kuanzia nyuma, hali iliyomruhusu Harvey Barnes kuiba mpira kabla ya kumtengenezea mwenzake nafasi ya kufunga.
Dakika nne baadaye mambo yakawa mabaya zaidi baada ya William Osula kufunga bao la pili na kuzamisha matumaini ya wageni.
Nuno alifanya mabadiliko ya haraka kwa kumtoa Jean-Clair Todibo na kumuingiza Taty Castellanos ili kuongeza nguvu ya ushambuliaji, lakini jitihada hizo hazikutosha.
Osula aliifungia Newcastle bao jingine baada ya makosa mengine ya West Ham, kabla ya Castellanos kufunga bao la kufutia machozi.
Matokeo hayo yanaifanya Tottenham kuwa na nafasi kubwa ya kubaki kwenye ligi na kuwashusha rasmi West Ham iwapo watashinda mchezo wao unaofuata.
Sasa West Ham wana pointi 36 zikiwa ni mbili nyuma ya Spurs ambao wana mchezo mmoja mkononi, endapo watashinda ina maana kuwa West Ham, Burley na Wolves watashuka daraja na Spurs itaokoka kwa msimu wa pili mfululizo.