Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Boli la Arsenal na utamu wa ubingwa EPL msimu huu

Muktasari:

  • Arsenal wako karibu kutwaa ndoo, kwani baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo, hivi sasa inaonekana kuna uwezekano mkubwa kwamba watatwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.

LONDON, ENGLAND: BAADA ya miaka 22 ya ukame wa mataji, Arsenal wako karibu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England unaokuja kutokana na mtindo wao wa mchezo ambao huenda usiwe maarufu kwa wengi, lakini mafanikio hayo yatakuwa uthibitisho kwa Mikel Arteta kwamba ameusotea vilivyo.

Arsenal wako karibu kutwaa ndoo, kwani baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo, hivi sasa inaonekana kuna uwezekano mkubwa kwamba watatwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.

Baadhi ya mashabiki huenda walikuwa wameanza kujiuliza kama Arteta angeweza kweli kuwavusha mstari wa mwisho, na hofu iliongezeka zaidi baada ya Arsenal kufungwa na Manchester City, Aprili 19, matokeo yaliyoonekana kuonyesha kwamba kikosi cha Pep Guardiola kilikuwa na kasi na nguvu, licha ya Arsenal kubaki kileleni mwa msimamo.

Lakini, tangu hapo, Arsenal wameshinda mechi zote tatu zilizofuata, huku sare ya kusisimua ya mabao 3-3 kati ya Manchester City na Everton ikibadilisha mwelekeo wa mbio za ubingwa kwa faida ya kikosi cha Arteta. Na sasa wakibakiwa na mechi dhidi ya Burnley walioshuka daraja nyumbani pamoja na safari ya kwenda kucheza na Crystal Palace ambao huenda wakawa wamevurugwa mawazo na fainali ya Conference League, Arsenal wanapewa nafasi ya asilimia 86.5 ya kutwaa ubingwa kulingana na makadirio ya kompyuta ya Opta yaliyofanywa mara 10,000.

Katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyopita, safari haijawahi kuwa rahisi, lakini kwa sasa Arteta yuko karibu kukamilisha mapinduzi ya Arsenal aliyokusudia kuyaanzisha Desemba 2019.

Ikiwa wataendelea kushikilia bomba hadi mwisho, shangwe katika Uwanja wa Emirates zitakuwa kubwa na Mhispania huyo ataheshimiwa kwa kukomesha ukame wa zaidi ya miongo miwili ya ukosefu wa taji la Ligi Kuu England.

Kwa wengi hata hivyo, mjadala kuhusu Arsenal huenda usiwe wa shauku kubwa kiasi hicho. Kwa mtazamo wa mtindo wa mchezo huenda wakawa miongoni mwa mabingwa wa Ligi Kuu England wasiopendwa zaidi kuwahi kutokea. Mashabiki wa Arsenal hawatajali hilo – na ni nani angelaumu? Lakini mjadala utaelekezwa haraka kwenye namna walivyofanikiwa kubeba taji.

Kama hujaishi chini ya mwamba, basi fahamu vizuri uwezo mkubwa wa Arsenal katika mipira ya adhabu na kona. Kwa muda mrefu, eneo hilo  lilikuwa halitumiki kikamilifu katika soka, lakini Arteta aligundua kwamba hapa ndipo timu yake ingeweza kupata faida ya kuziba pengo dhidi ya timu bora zaidi.

Tangu hapo, kona zimekuwa silaha kubwa zaidi na wamekuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya mipira ya adhabu Ligi Kuu England. Wapo watu wanaoamini kwamba kuzingatia sana mipira ya adhabu kumepunguza ubora wa burudani ya soka na kufanya mchezo usivutie sana. Lakini hakuna anayeweza kusema kwamba mbinu hiyo haijawa na mafanikio.

Katika misimu mitatu iliyopita kwa mfano, Arsenal wamefunga mabao 60 Ligi Kuu England kupitia kona, ikiwa ni mabao 11 zaidi ya timu yoyote nyingine. Tottenham Hotspur wanafuata kwa mabao 49, huku West Ham United na Liverpool wakiwa na mabao 39 kila mmoja katika kipindi hicho. Hii inaonyesha jinsi Arsenal walivyo bora zaidi kuliko wengine katika eneo hilo.

Lakini, pia kuna mtazamo kwamba ufanisi katika mipira ya adhabu umeathiri kiwango chao cha kucheza mpira wa wazi (open play).

Katika msimu huu, mabao 41 ya open play hayaonekani kuwa bora vya kutosha ukizingatia kwamba ni Liverpool (43) na Manchester City (62) pekee waliofunga zaidi yao. Kinachoshangaza zaidi ni rekodi yao ikilinganishwa na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu England ni mbingu na ardhi kwani wenzao walikuwa wanafunga mabao makali yenye kusisimua mashabiki. Pia Arsenal wamekuwa wakifunga wastani wa mabao 1.08 ya wazi kwa kila mchezo msimu huu, ingawa wastani huo unaweza kubadilika kidogo, lakini katika michezo miwili iliyobaki.

Takwimu zinaonyesha kwamba Arsenal wako mbioni kuweka rekodi mpya ya chini kabisa kwa mabingwa wa ligi hiyo ya mabao 1.08 ambayo ajabu miongoni mwa timu zilizowahi kutwaa ndo hiyo. Rekodi iliyopo kwa sasa ni ya Manchester United katika msimu wa kwanza wa Ligi Kuu England 1992-93 walipobeba ubingwa wakiwa na wastani wa mabao 1.17 ya 'open play' kwa kila mchezo.

Ili Arsenal wasimalize msimu wakiwa chini ya kiwango hicho wanahitaji kufunga angalau mabao manne ya 'open play' katika mechi mbili zilizobaki. Hilo litawawezesha kumaliza msimu wa 2025-26 wakiwa na wastani wa mabao 1.18 kwa kila mchezo. Kimsingi, wanahitaji kufunga mabao ya wazi kwa kiwango mara mbili ya kile walichofanya katika mechi 36 za kwanza za msimu.


VS MABINGWA WA KARIBUNI

Timu ya mwisho kushinda ubingwa ikiwa na wastani wa chini ya mabao 1.5 ya 'open play' kwa kila mchezo ilikuwa Leicester City 2016 iliyokuwa na 1.21. Tangu hapo, mabingwa wamekuwa wakifunga wastani wa mabao 1.84 ya wazi kwa kila mchezo kuanzia Chelsea 2016-17 (mabao 1.61) hadi Manchester City 2017-18 (2.24), ambayo ndiyo rekodi ya ligi.

Arsenal pia wako mbioni kuweka rekodi ya chini zaidi ya jumla ya mabao ya 'open play' kwa mabingwa wa ligi, wakihitaji matano zaidi ili kufikia 46 yaliyofungwa na Leicester City miaka 10 iliyopita. Kwa kulinganisha, Liverpool walifunga mabao 67 ya wazi walipobeba ubingwa msimu uliopita.

Kwa upande mwingine, Arsenal wako kileleni kabisa linapokuja suala la ufanisi wa mabao ya mipira ya adhabu kwa mabingwa wa ligi. Ikiwa hawatafunga tena kupitia mipira ya adhabu (ukiondoa penalti), mabao yao 23 yatakuwa sawa na rekodi ya mabao mengi zaidi ya 'set-pieces' yaliyofungwa na mabingwa wa Ligi Kuu England, rekodi inayoshikiliwa na Manchester United msimu wa 2012-13.

Iwapo Arsenal watafunga bao moja zaidi la 'set-piece' wataweka rekodi mpya kabisa ya jumla ya mabao hayo pamoja na wastani kwa kila mchezo. Kama ilivyoelezwa uwezo wa Arsenal kwenye kona umejenga hofu kubwa kwenye mipira ya adhabu kwa wapinzani wao, na  inaonekana wana mchanganyiko bora wa wapigaji bora wa mipira hiyo, wachezaji wenye uwezo mkubwa wa mipira ya juu pamoja na kocha mahiri wa 'set-pieces', Nicolas Jover.

Huu siyo msimu wa bahati kwao, kwani mabao 17 ya kona tayari yamevunja rekodi ya ligi hiyo kwa timu yoyote katika msimu mmoja. Takwimu zinaonyesha Arsenal wako mbioni kuwa mabingwa waliotegemea zaidi 'set-pieces' kuliko timu yoyote nyingine katika historia ya ligi.

Lakini je, hilo lina umuhimu wowote? Tatizo la Arsenal kufunga mabao machache ya 'open play' siyo jambo jipya, na wakati mwingine limetumiwa kudhoofisha uhalali wa mbio zao za ubingwa. Lakini ukweli kwamba ni timu mbili tu zimefunga mabao mengi zaidi ya 'open play' kuliko wao unaonyesha kuwa hilo ni tatizo la ligi nzima, na siyo Arsenal pekee. Kwa ujumla, Ligi kuu England imekuwa na wastani wa mabao 1.8 ya wazi kwa kila mchezo msimu huu kikiwa ni kiwango cha chini zaidi tangu 2009-10.

Wakati huohuo, wastani wa mabao ya 'set-pieces' ni mkubwa kuliko kawaida. Huenda hayo yote yanaonyesha kupungua kwa burudani na ubora wa soka katika ligi hiyo msimu huu. Na inawezekana Arsenal wamechangia mabadiliko hayo kwa sababu timu nyingine kuona mafanikio yao na kuanza kuiga mbinu zao.

Lakini je, hilo linaifanya iwe tatizo? Ukweli ingekuwa vizuri kama kila mechi ingekuwa ya kusisimua na yenye mashambulizi ya kuvutia, lakini hivyo sivyo soka lilivyo. Soka hubadilika kila wakati; nyakati hubadilika, mitindo huja na kuondoka.

Enzi za Pep Guardiola dhidi ya Jurgen Klopp (Liverpool) zilizalisha misimu mingi ya kuvunja rekodi, lakini vipindi kama hivyo haviwezi kudumu milele. Arteta ameiweka Arsenal katika nafasi nzuri ya kutumia pengo la nguvu lililoonekana kuja juu. Uamuzi wake wa kuona 'set-pieces' zinaweza kuwasaidia kufika huko haumfanyi kuwa adui wa mchezo wa soka, bali unaonyesha kwamba yeye ni kocha mzuri.

Guardiola alisifiwa kwa kuleta mabadiliko makubwa katika ligi hiyo alipowasili Manchester City. Takwimu za msimu huu zinaonyesha kwamba Arteta pia amefanya jambo kama hilo, au angalau amekuwa mmoja wa makocha wa mabadiliko hayo ya kimtazamo. Ni muda tu ndio utaamua kama mabadiliko hayo yatadumu kama yale yaliyoletwa na Guardiola.

Lakini, bila kujali kama watu wanafurahia kuangalia Arsenal au la, Arteta yuko karibu kufanya kile ambacho hakuna kocha mwingine wa Arsenal amefanya kwa miaka 22 yaani kushinda Ligi Kuu England. Huo pekee ni uthibitisho tosha.