West Ham, Nuno mambo yamenyooka
Muktasari:
- Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo, bodi ya wakurugenzi imeeleza kuwa ingawa kushuka daraja ni jambo lenye maumivu makali, mipango ya msimu ujao imeanza mara moja chini ya kocha huyo raia wa Ureno.
Uongozi wa klabu ya West Ham United umethibitisha kocha Nuno Espirito Santo ataendelea kuinoa timu hiyo kwa lengo la kuirejesha Ligi Kuu ya England msimu ujao.
Nuno alichukua mikoba ya Graham Potter mwezi Septemba wakati timu hiyo ikiwa tayari kwenye mapambano ya kujinasua kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi. Licha ya kufanya mabadiliko makubwa na kuziba pengo la pointi nane, ushindi wa Spurs dhidi ya Everton katika mechi ya mwisho uligeuka kuwa pigo kwa klabu hiyo ya masharinbi mwa London.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo, bodi ya wakurugenzi imeeleza kuwa ingawa kushuka daraja ni jambo lenye maumivu makali, mipango ya msimu ujao imeanza mara moja chini ya kocha huyo raia wa Ureno.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Nuno ameonesha nia thabiti na ari kubwa ya kuiongoza West Ham kurudi kwenye ligi kuu ifikapo mwezi Agosti 2027, huku uongozi ukiamini kuwa kuna dalili kubwa za maendeleo ya kiuchezaji yaliyoonekana chini ya kocha huyo katika miezi ya hivi karibuni, jambo linalomfanya astahili kuendelea na mradi huo.
Ili kupunguza hasira za mashabiki, West Ham pia imetangaza kupunguza bei za tiketi za msimu ujao kwa asilimia 30. Hatua hii inakuja baada ya mechi ya mwisho dhidi ya Leeds kukumbwa na vurugu na nyimbo za kashfa kutoka kwa mashabiki zilizomlenga mmiliki wa klabu, David Sullivan, hali iliyomfanya aondoke uwanjani mapema.
Hata hivyo, baada ya taarifa hiyo ya bodi na punguzo la bei, baadhi ya mashabiki wameonekana kuridhishwa na kauli hiyo kwenye mitandao ya kijamii, huku wakisifu kuwa ni moja ya taarifa zenye busara zaidi kuwahi kutolewa na uongozi wao.
Kwa upande mwingine, mabadiliko makubwa yanatarajiwa nje na ndani ya uwanja kwani klabu inalenga kukusanya kiasi cha pauni milioni 150 kupitia mauzo ya wachezaji.
Aaron Wan-Bissaka anawaniwa na Newcastle na Everton kwa dau la pauni milioni 10 (Sh35.2 bilioni), huku Mateus Fernandes akiwa kwenye rada za Manchester United, ingawa Jarrod Bowen ameeleza nia yake ya kubaki.
Mabadiliko hayo ya kikosi yanakuja huku klabu ikiwa tayari imeshuhudia kuondoka kwa Makamu Mwenyekiti Karren Brady na nafasi yake kuchukuliwa kwa muda na Karim Virani kama Afisa Mtendaji Mkuu (CEO).