Wembanyama anavyopita njia ya LeBron
Muktasari:
- Wembanyama kutoka Ufaransa, anaendelea kuthibitisha kuwa na kipaji kinachoweza kubadilisha historia ya mpira wa kikapu duniani. Kwa sasa anaonekana kuwa katika kiwango cha juu ambacho ni vigumu kwa wapinzani kumdhibiti uwanjani.
TEXAS, MAREKANI: HAKUNA ubishi kuwa Victor Wembanyama ni kati ya wachezaji chipukizi wanaoibeba sura mpya ya NBA akivunja rekodi kibao na kuonyesha bora kinachowafanya baadhi ya wachambuzi kumlinganisha na supastaa wa michuano hiyo, LeBron James.
Wembanyama kutoka Ufaransa, anaendelea kuthibitisha kuwa na kipaji kinachoweza kubadilisha historia ya mpira wa kikapu duniani. Kwa sasa anaonekana kuwa katika kiwango cha juu ambacho ni vigumu kwa wapinzani kumdhibiti uwanjani.
Kila mchezo anaocheza unaonyesha mabadiliko makubwa katika uelewa wake wa mchezo, jambo linalomfanya kuwa tishio katika pande zote mbili, ushambuliaji na kulinda. Kadri anavyoendelea kukua na kuongeza ubora wake, timu yake ya San Antonio Spurs imekuwa ikipata ushindi mfululizo, hali iliyowasukuma kuwa miongoni mwa timu bora ligi. Kwa sasa ambapo wanashindana na Oklahoma City Thunder katika mbio za kuwa na rekodi bora zaidi msimu huu.
MAFANIKIO YA MAPEMA
Katika umri mdogo sana, Wembanyama tayari anamafanikio ambayo wachezaji wengi huyafikia kwa miaka mingi. Amekuwa mchezaji wa kwanza katika kipindi cha miaka 40 kufikisha zaidi ya pointi 4,000 na mizuio ‘blocks’ 600 kabla ya kufikisha miaka 23.
Mbali na hilo, alionyesha uwezo mkubwa kwa kufunga pointi 41 katika mchezo mmoja idadi kubwa zaidi kwake msimu huu pamoja na mipira ya kurudi ‘rebounds’ 16. Mafanikio hayo yaliisaidia Spurs kufikisha rekodi ya ushindi 57-18, hali inayothibitisha mchango wake mkubwa kwa timu.
Akizungumzia maendeleo yake, alisema: “Ninaendelea kujifunza na kuboresha mchezo wangu. Nilihitaji kurudisha kiwango changu cha kushambulia bila kupunguza uimara wangu wa kulinda.”
TUZO YA MVP
Kadri msimu wa NBA unavyokaribia mwisho, jina la Wembanyama limekuwa miongoni mwa majina yanayotajwa sana katika kinyang’anyiro cha tuzo ya MVP. Anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushindana na mastaa wakubwa wa ligi hiyo. Anashindana na wachezaji kama Luka Doncic, Nikola Jokic na Shai Gilgeous-Alexander, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitawala mijadala ya ubora katika NBA.
MRITHI WA LEBRON
Wengi wanaamini kuwa Wembanyama ndiye mchezaji bora chipukizi tangu kuibuka kwa LeBron James. Kama ilivyokuwa kwa LeBron mwanzoni mwa maisha yake katika mchezo, Wembanyama anaonyesha uwezo wa kubeba timu, kumaliza mchezo na kuvutia mashabiki duniani kote. Baada ya kuchaguliwa kama namba moja mwaka 2023, alitwaa tuzo ya Rookie of the Year yani mchezaji bora ambaye kwa mara ya kwanza anacheza NBA na baadaye akachaguliwa kushiriki mchezo wa All-Star mwaka 2025.
Pia aliiongoza NBA kwa ‘blocks’ katika misimu yake miwili ya kwanza, licha ya kukumbwa na changamoto ya kiafya iliyomfanya kusimamishwa katika msimu wake wa pili.
THAMANI YAKE SOKONI
Katika hatua za mwanzo katika uchezaji wake wa mpira wa kikapu, Wembanyama alisaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya dola 55milioni na Spurs.
Kwa sasa anapata wastani wa dola 13.8 milioni kwa mwaka lakini matarajio ni kwamba mapato yake yataongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ijayo.
Kuanzia mwakani, anaweza kusaini mkataba mpya wa hadi dola 271 milioni au hata dola 326 milioni ikiwa atapata mafanikio makubwa kama MVP au tuzo nyingine za juu.
MIKATABA YA KIBIASHARA
Umaarufu wa Wembanyama hauko tu uwanjani, bali pia nje ya uwanja. Ameshavutiwa na makampuni makubwa duniani na kusaini mikataba yenye thamani kubwa.
Miongoni mwa makampuni hayo ni Nike, ambayo inasemekana ilimpa mkataba wa zaidi ya dola 100 milioni. Pia ni balozi wa Louis Vuitton, pamoja na kushirikiana na Fanatics na 2K Sports.
ASILI YAKE
Wembanyama alizaliwa Ufaransa na kukulia katika mazingira yenye misingi ya michezo. Baba yake alikuwa mwanariadha huku mama akiwa mchezaji na kocha wa kikapu.
Mama yake ndiye aliyemfundisha misingi ya mchezo huo tangu akiwa mdogo na kumsaidia kukuza kipaji chake hadi kufikia kiwango cha juu. Kabla ya kutua NBA alicheza katika ligi mbalimbali za Ulaya na kuwa mmoja wa wachezaji wadogo zaidi kushiriki mashindano ya EuroCup.
Hapa ni takwimu za Wembanyama dhidi ya LeBron katika msimu wa kwanza na wa pili kwa mechi.