Welbeck apita njia ya Ibrahimovic EPL
Muktasari:
- Ni Zlatan Ibrahimovic na Gary McAllister pekee waliowahi kufanikisha hilo awali na wote wawili walikuwa na miaka 35 walipovunja rekodi ya mabao 10, huku Ibrahimovic akifunga mara 17 akiwa na Manchester United 2016/17.
BRIGHTON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Brighton, Danny Welbeck amefanikiwa kufikia jambo ambalo ni wachezaji wawili tu wengine katika historia ya Ligi Kuu England wamewahi kulifanya, baada ya kufunga dhidi ya Liverpool.
Straika huyo alifunga mabao mawili dhidi ya Liverpool katika Uwanja wa Amex mwishoni mwa wiki iliyopita na kufikisha mabao 12 msimu huu, na hiyo imemfanya kuwa mchezaji wa tatu katika historia kufunga zaidi ya mabao 10 katika msimu akiwa na umri wa miaka 35 au zaidi.
Ni Zlatan Ibrahimovic na Gary McAllister pekee waliowahi kufanikisha hilo awali na wote wawili walikuwa na miaka 35 walipovunja rekodi ya mabao 10, huku Ibrahimovic akifunga mara 17 akiwa na Manchester United 2016/17.
Kwa upande mwingine, McAllister alifunga mabao 11 akiwa kiungo kwa Coventry City msimu wa 1999/2000, lakini kwa Welbeck mbali na kuungana na wakali hao pia ameweka rekodi binafsi.
Bao lake la 12 la ligi hiyo msimu huu linamaanisha kuwa sasa ameweka rekodi yake ya juu zaidi ya mabao katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England.
Licha ya kuwa na miaka 17 ya kucheza katika ligi hiyo, akipita Manchester United na Arsenal, Welbeck ameonyesha ubora mkubwa katika misimu miwili ya mwisho.
Alifunga mabao 10 kwa Brighton msimu uliopita, huku kiwango chake msimu huu kikimfanya apewe nafasi ya kurejea katika timu ya taifa ya England.
Hata hivyo, mkongwe huyo hajajumuishwa katika kikosi cha wachezaji 35 kilichotangazwa na kocha Thomas Tuchel kwa ajili ya mapumziko ya mechi za kimataifa kilichowekwa hadharani katikati ya wiki iliyopita.