Weah ashindwa urais Liberia, ampongeza mpinzani wake

MONROVIA, LIBERIA. MGOMBEA wa urais na mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Liberia na timu ya AC Milan ya Italia , George Weah amempigia simu mpinzani Joseph Boakai (78) na kumpongeza kwa ushindi wake baada ya kushinda kiti cha urais.

Weah (58) aliyekuwa akitetea kiti hicho kupitia Chama cha Congress for Democratic Change alishinda urais wa nchi hiyo mwaka 2018.

Hata hivyo ameshindwa kwa tofauti ya kura 28,000 na Boakai, mgombea wa chama cha upinzani cha Unity Party.
Kabla ya kushindwa kiti cha urais, Weah amekuwa madarakani tangu 2018 na ataondoka madarakani itakapofika Januari, mwakani.

Awali, wakati wa kampeni Weah alitamba kunyakua ushindi hasa ukizingatia kwamba alitegemea kura nyingi kutoka kwa vijana ambao walikuwa wakimuunga mkono kutokanana kucheza kwake soka ngazi ya kimataifa.

Imeelezwa kwamba Weah ameshindwa uchaguzi wa urais kwa sabbau amefeli kukabiliana na ufisadi, kupanda kwa bei ya vyakula na matatizo ya kiuchumi yaliyomharibia sifa yake.

Akizungumza kwenye hotuba yake iliyodumu kwa dakika tano kumpongeza mpinzani wake, nyota huyo aliyewahi pia kuzichezea PSG, Manchester City, Monaco na Marseille amesema anaheshimu sana mchakato wa kidemokrasia ambao umelifanya taifa hilo liwe na uhuru mkubwa kwa watu wake baada ya kupitia kipindi kirefu cha vita kabla ya kurejea kwa demokrasia miaka 18 iliyopita.

Tume ya uchaguzi ilitangaza kuwa Boakai, mkongwe wa kisiasa na makamu wa rais wa serikali ya kabla ya Weah iliyoongozwa na Ellen Sirleaf alikuwa na asilimia 50.89 ya ushindi huku Weah akiwa na 49.11.

Baada ya matokeo kutangazwa watu wameipuka kwa furaha na kufanya sherehe katika mji mkuu, Monrovia ambapo wafuasi wa Boakai walikusanyika katika makao makuu ya chama chake mjini humo.