WATAWEZA? Wanasubiriwa kurudisha, kuweka heshima 2024

NI siku ya tatu baada ya Mwaka Mpya 2024. Msimu wa michezo unazidi kupamba moto na wanamichezo wanazidi kujipanga kwa mwaka huu kuona hadi Desemba watakuwa wamefanya nini. Kila mtu anataka kuanza mwaka vizuri.

Mapema tu Januari hii michuano ya wazi ya Australia (Australia Open) itaanza. Tarehe 24-28. Kivumbi kitatimka.

Ni moja ya mataji makubwa ya tenisi duniani. Kila mmoja analitolea macho.

Kwenye masumbwi, Februari 27. Sio mbali. Kivumbi kingine kati ya Tyson Fury na TOleksandr Usyk. Nani atakaa? Tusubiri tuone.

Mbio za magari ya langalanga. Huku ndo vumbi lenyewe. Ni Februari hiyo hiyo, huku kwenye mpira wa kikapu, NBA ikizidi kuchanja mbuga. Mwaka unaanza kibabe.

Hata hivyo, kwenye mikikimikiki hiyo, kuna waliomaliza mwaka kwa furaha na wengine wanaangalia namna gani watauanza kwa shangwe ili wawe na msimu mzuri. Kazi wanayo.

RAFAEL NADAL

Mara ya mwisho aliumia kwenye raundi ya pili ya michuano ya Australia, Januari mwaka jana na mwaka huu itafanyika Melbourne. Staa huyu Mhispania, anarudi tena kujaribu kurudisha taji hilo alilolipoteza mwaka jana kwa mpinzani wake mkubwa Novak Djokovic wa Serbia.

Nadal ana mataji 22 makubwa ya tenisi (Grand Slam) kutokana na ubora mkubwa aliokuwa nao. Sasa ana kazi nzito sana ya kuhakikisha anamfikia Djokovic mwenye mataji 24 na ili amfikie anatakiwa kuanza na taji la Australia na baada ya hapo kuna mataji manne yajayo, Rolland Garros la Ufaransa, Wimbledon la Uingereza, US Open la Marekani na taji la olimpiki.

Umri unamtupa mkono. Ndiyo mwaka pekee wa kujua hatma yake katika kujikusanyia mataji makubwa. Majeraha pia yamekuwa sababu ya kurudi nyuma, lakini anaweza kupambana na kutwaa mataji hayo matano au hata matatu nakurudiusha heshima yake.


TYSON FURY

Ana umri wa miaka 15. Ni mingi kwa bondia kuwa ulingoni. Ila kwa Fury, bado sana. Hii ni sababu ya Fury kutaka kuutumia mwaka huu kufanya makubwa.

Moja ya mambo hayo ni kuweka rekodi ya kutopigwa endapo atastaafu na kushikilia mkanda wa WBC uzito wa juu (heavyweight), tangu alipouchukua mikononi mwa Deontay Wilder 2021.

Ili kufanikisha hayo, ana kibarua mwezi Februari dhidi ya Usyk na lile la marudiano baadaye itakapopangwa.

Fury anashikilia rekodi yake ya kupigana mapambano 35 bila kupigwa akitoa droo moja tu dhidi ya Wilder.

Usyk ndio alimnyang’anya mikanda yote mitatu bondia Anthony Joshua kwenye mapambano mawili mtawalia akishinda kwa pointi za majaji wote watatu, hivyo anaweza kuwa shubiri pia kwa Fury kama hatajipanga vyema kulingana na pambano lake la mwisho dhidi ya Francis Ngannou kuonekana amepungua makali.

LEWIS HAMILTON

Dereva mwingereza wa mbio za magari ya langalanga (formula one) ambaye hajawa na ubora kwa miaka ya karibuni, baada ya kutamba kwa miaka saba akitwaa mataji saba sawa na gwiji Michael Schumacher wa Ujerumani.

Kwa miaka miwili hajashinda mbio zozote. Mwaka huu utaamua hatma yake ya kama anaweza kuivuka rekodi hiyo na kuwa bingwa mara nane au ataendelea kusota mbele ya bingwa wa sasa, Max Verstappen wa Uholanzi aliyeshinda mbio 18 katika 22 za msimu mzima.

Akitumia magari ya Kampuni ya Mercedes, ana kazi nzito mwaka huu kurudisha heshima yake.

JOEL EMBIID ‘MVP’

Tuzo ya mchezaji mwenye thamani zaidi ya NBA ‘MVP’ inashikiliwa na Joel Embiid. Msimu huu wa ligi ndefu (regular season) bado haina mwenyewe na vita ni kubwa.

Mwa miaka mitatu iliyopita vita ilikuwa kali na mwaka huu ni kutokana na aina ya wachezaji wanaowania na misimu minne sasa, wachezaji watatu wameendelea kukimbizana kwenye uwezekano mkubwa wa kuichukua tuzo hiyo kubwa zaidi kwa mchezaji NBA.

Embiid anarejea tena kwenye kinyang’anyiro akichuana na  Giannis Antetokounmpo na Nikola Jokic walioibeba mara mbili mbili mtawalia kabla ya Embiid kuibeba mwaka jana.

Embiid ambaye anaongoza kwenye uwezekano wa kuibeba tena msimu huu, mwaka huu ana kazi kubwa ya kuifanya mbele ya Giannis, Jokic na Luka Doncic wanaomfukuzia kwa ukaribu na itatolewa kabla ya fainali ya jumla ya NBA kati ya bingwa wa Mashariki na Magharibi. Tusubiri tuone.