Wapo na simu zao mkononi wakisubiri mchongo

Muktasari:

  • Miamba kama Barcelona, Bayern Munich, Chelsea ipo sokoni kusaka makocha wapya wa kwenda kuchukua majukumu ya kunoa timu hizo kwa ajili ya msimu ujao.

LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu za Ulaya zimeshafika mwisho na sasa klabu kubwa kibao zinapiga hesabu za kunasa makocha wapya ili kurudi kivingine msimu ujao wa 2024/2025.

Miamba kama Barcelona, Bayern Munich, Chelsea ipo sokoni kusaka makocha wapya wa kwenda kuchukua majukumu ya kunoa timu hizo kwa ajili ya msimu ujao.

Liverpool yenyewe imeshamalizana na jambo hilo baada ya kumnasa Mdachi Arne Slot, anayekwenda Anfield kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp, aliyeachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu, akiacha na taji la Kombe la Ligi na tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutokana na kuwapo kwa mahitaji makubwa ya makocha, na kitu kizuri ni kwamba wapo ambao hawana kazi hadi sasa, bila shaka simu hazitaishiwa chaji kwani waalimu hao sasa wanasikilizia mchongo wa kupewa ajira kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.


10. Andre Villas-Boas

Pengine ajira ya Andre Villas-Boas kwenye timu kubwa inaweza kuwa na shaka kubwa baada ya kushindwa kufanya vizuri alipopita kwenye timu za Chelsea na Tottenham, lakini jambo hilo halimfanyi kuzima simu zake kwenye ishu ya kusikilizia kazi kwenye kipindi hiki, ikiwa alifanya kazi pia kwa mafanikio makubwa huko Russia na China kabla ya kuhamia Marseille mwaka 2019.

Huko Marseille alikuwa na matatizo ya nje ya uwanja, lakini uwanjani kikosi chake kilicheza soka la kibabe sana, akioongoza timu hiyo kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita. Alipoondoka kiti chake kilichukuliwa na Jorge Sampaoli, ambaye pia hakudumu muda mrefu. Kwa sasa, AVB hana kazi, anasubiri mchongo.


9. Joachim Low

Joachim Low ni jina kubwa kwenye tasnia ya makocha wa mchezo wa mpira wa miguu duniani na mafanikio yake makubwa amepata kwenye soka la kimataifa. Amekuwa hana kazi tangu mwaka 2021. Low, 63, alifika fainali tatu za michuano mikubwa katika kipindi chake cha miaka 15 aliyokuwa kocha wa Ujerumani na mwaka 2014 alinyakua Kombe la Dunia katika fainali zilizofanyika Brazil, huku akishinda pia fainali ya Kombe la Mabara 2017, akifika fainali ya Euro 2008 na nusu fainali ya Kombe la Dunia 2010, ambako alimaliza nafasi ya tatu. Kwenye soka la ngazi ya klabu, alifanya vizuri zaidi kwenye msimu wa 2001/02, alipobeba ubingwa wa Austrian Bundesliga alipokuwa na kikosi cha Tirol Innsbruck na alinyakua DfB-Pokal akiwa na Stuttgart ya Ujerumani.


8. Graham Potter

Graham Potter CV yake ilitibuka kiasi baada ya kushindwa kufanya vyema huko Stamford Bridge, ambako alikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 39 tu, ikiwa ya chini sana kwenye historia ya makocha wa Chelsea. Lakini, nyakati zake alizokuwa A–stersunds FK, Swansea na Brighton zilikuwa moto sana na kumfanya aendelee kuwa kocha anayesakwa na timu nyingi vigogo zikihitaji kufanya naye kazi. Mbinu zake za ufundishaji na namna soka linalochezwa na timu zake ndicho kitu kinachomfanya kocha huyo bado ahusishwe na timu kubwa licha ya kufanya hovyo alipokuwa na Chelsea. Alifanya kazi nzuri sana huko Brighton na kuifanya timu hiyo ya Amex kuwa tishio kwa timu nyingi zilizokwenda uwanjani hapo kucheza mechi kwenye Ligi Kuu England.


7. Ole Gunnar Solskjaer

Solskjaer nyakati zake alizokuwa Manchester United zimeachana kumbukumbu nyingi za kushangaza. Straika huyo wa zamani wa Mashetani Wekundu alipewa muda kwenye kikosi hicho, ambapo alimaliza miaka mitatu kabla ya kufunguliwa mlango wa kutokea. Na hakika, hakuwa na wakati mbaya sana, ambapo aliondoka akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 54.17 na aliifikisha timu kwenye fainali ya Europa League mwaka 2021. Baadaye, mambo yalitibuka na kumfanya Solskjaer aonekane kama hana ujuzi wa kutosha wa kufundisha klabu kubwa na zenye malengo makubwa kama Man United. Hata hivyo, kwa kile alichofanya Old Trafford, bado kinamfanya ahesabike kama mmoja wa makocha wanaofaa kupewa kazi kipindi hiki.


6. Massimiliano Allegri

Juventus iliamua kuachana na Massimiliano Allegri katika awamu yake ya pili katika timu hiyo baada ya kumfuta kazi kufuatia kile alichofanya kwenye fainali ya Coppa Italia. Ikiwa zimepita siku mbili tangu alipoisaidia Juventus kuibuka na ushindi, Allegri aliadhibiwa baada ya kutibuana na waamuzi na pia kumsukuma mkurugenzi wa michezo wa Juventus kwenye tukio la kushangilia. Kutokana na hilo, shirikisho la soka la Italia lilipeleka shauri lake kwa kamati ya nidhamu kwa uchunguzi zaidi. Katika awamu yake ya kwanza Juventus, Allegri aliinoa timu hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi 2019, na alishinda mataji kwa misimu yote mitano na alifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili. Awamu yake ya pili Juventus haina mafanikio makubwa.


5. Hansi Flick

Kwenye karatasi kila kitu kinaonekana kuwa vizuri baina ya Hansi Flick na timu anayoinoa ya Ujerumani. Wakati Ujerumani inachukua ubingwa wa Kombe la Dunia 2024, Flick alikuwa kocha msaidizi na sasa amekabidhiwa timu hiyo baada ya kunyakua Bundesliga kwa misimu miwili mfululizo na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Bayern Munich, ambako alipata mafanikio makubwa, akiwa amepoteza mechi saba tu kati ya 86. Baada ya kuanza vizuri ajira yake kwenye timu ya taifa ya Ujerumani, mambo yalikwenda kuwa kombo kwenye Kombe la Dunia 2022, ambapo timu hiyo ilikomea kwenye hatua ya makundi, huku ikichapwa kwa dharau mabao 4-1 na Japan. Na sasa Flick anaweza kurudi kwenye soka za klabu, kutokana na timu kibao kuhitaji huduma yake.


4. Mauricio Pochettino

Hakuna ambaye alidhania kabisa kama Mauricio Pochettino ataingia kwenye kundi la makocha wasiokuwa na ajira kwa sasa baada ya kupewa kazi mwaka jana tu, alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa Chelsea. Maisha yake huko Stamford Bridge yalianza vibaya, ambapo The Blues ilikuwa haijielewi hadi hapo dakika za mwisho za msimu, ambapo ilipambana na kumaliza kwenye nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England. Nafasi hiyo iliifanya Chelsea kufuzu kucheza Europa League, kabla ya tiketi hiyo kubebwa na Man United baada ya kubeba ubingwa wa Kombe la FA. Pochettino ni miongoni mwa makocha wenye majina makubwa, ambao bila ya shaka kwenye dirisha hili mezani kwake kutakuwa na ofa kibao za kumtaka akapige kazi kwingine.


3. Antonio Conte

Mtaliano, Antonio Conte alitua Tottenham katika staili ya aina yake na aliacha kazi kwenye timu hiyo kwa staili hiyo hiyo. Kwa sasa hana kazi. Lakini, kitu ambacho hakuna anayepinga ni kwamba, Conte ni kocha anayefahamu namna ya kubeba mataji, kitu ambacho kinampa nafasi kubwa ya kupata kazi. Alionyesha ubora mkubwa alipopita kwenye timu za Chelsea, Juventus, Inter na Bari, ambako kote huko alizipa mataji timu hizo. Ni Spurs tu ndio mahali ambako Conte alishindwa kuonyesha ubora wake na kubwa alidai kwamba bosi wa timu hiyo, Daniel Levy kuna mambo mengi ya kimpira hafanyi, huku akiwashutumu wachezaji wa Spurs kwamba hawachukizwi na kitendo cha kucheza miaka yote bila ya kunyakua taji lolote.


2. Jose Mourinho

Jose Mourinho amejikuta tu hana timu hadi sasa. Hakuna ambaye hafahamu kuhusu ubora wa Mreno huyo, akipata mafanikio kwenye nchi zote kubwa kisoka, kuanzia England, Hispania, Italia na Ureno. Amebeba makombe kibao, ikiwamo yote ya Ulaya, ambapo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, Europa League mara mbili na Europa Conference League mara moja. Amebeba taji la ligi ya Ureno, England, Italia na Hispania. Kwa sasa jina lake linahusishwa na mpango wa kurudi Chelsea kwa awamu ya tatu, lakini Mourinho ni miongoni mwa makocha ambao bila shaka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, simu zao zitaita sana kutoka kwa timu zinazohitaji huduma zao kuanzia Ulaya hadi kwa timu za Saudi Arabia, ambazo zinaripotiwa kumtaka Mreno huyo.


1. Zinedine Zidane

Hana timu tangu alipoachana na Real Madrid. Lakini, taarifa za hivi karibuni ni kwamba, Zinedine Zidane yupo tayari kurudi kazini, anatafuta kazi kwa sasa, huku klabu kibao ikiwamo za Ligi Kuu England, Ligue 1 na Serie A zinaripotiwa kuhitaji huduma yake.

Katika kipindi chake alichokuwa na Real Madrid, alibeba La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo. Kabla ya hapo, hakukuwa na kocha yeyote aliyewahi kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Zidane kuonyesha ubabe wake, alinyakua taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo.  Tangu alipoachana na Los Blancos kwenye msimu wa 2020/21, ambako Zidane aliondoka mwenyewe baada ya kudai mabosi wa Madrid hawakuwa wakimwonyesha imani juu yake, Zizou hana ajira anasubiri simu iite.