Wanatoboa! Ugumu wa pointi 33 za ubingwa Arsenal

Muktasari:


LONDON, ENGLAND. KKOCHA, Mikel Arteta ameshinda mechi yake ya 100 tangu alipochukua mikoba ya kuinoa Arsenal wakati chama lake lilipoichapa Fulham 3-0 uwanjani Craven Cottage wikiendi iliyopita na kuweka pengo la pointi tano kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Ushindi huo ulikuwa na maana kubwa kwa Arteta, akifikisha karne moja ya ushindi tangu awe kocha wa miamba hiyo ya Emirates, Desemba 2019.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Arsenal, Arteta amefikisha idadi hiyo ya ushindi mara 100 baada ya kucheza mechi 168 ikiwa ni sawa na wastani wa asilimia 59.52 ya ushindi.

Kwa takwimu hizo, Arteta kama ataendelea na rekodi zake tamu hadi atakapoondoka, basi ataingia kwenye kitabu cha kihistoria na kuwa mmoja kati ya makocha mahiri kabisa waliowahi kutokea kwenye klabu hiyo ya Emirates.

Arteta ameshachukua taji la Kombe la FA na msimu huu mpango wake ni kunyakua taji la Ligi Kuu England kutokana na kikosi chake kuongoza ligi kwa muda mrefu na bado kuna mechi 11 tu za kumalizia.

Mara ya mwisho Arsenal ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa msimu wa 2002-2004, karibu miaka 19 iliyopita – hivyo msimu huu ikiwa kileleni kwa tofauti na pointi tano dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City, inamaini kama itaendelea kulinda pointi zake na kubaki juu kwa mechi 11 zijazo, basi itabeba taji hilo.

Lakini, kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, ambao ni mahasimu wakuu wa Arsenal, Jamie O’Hara amesema The Gunners haichukui, huku akizitaja siku saba ngumu ambazo anaamini ndizo zilizoshikilia hatima ya ubingwa wa miamba hiyo ya Emirates kwa msimu huu.

Na kwenye msisitizo wake wa kuhusu Arsenal kuwa haichukui ubingwa msimu huu, O’Hara alisema Man City itatetea taji lake kwa sababu Arteta na wachezaji wake hawataweza kuhimili presha hadi mwisho.

Arsenal inakabiliwa na ratiba ngumu sana mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei, wakati itakapokuwa na mechi dhidi ya Man City, Newcastle United, Chelsea pamoja na Brighton, huku mechi hizo tatu za kwanza, zikitofautiana kwa siku saba tu.

O’Hara alisema: “Nadhani Man City itachukua. Kwa sasa Arsenal ipo juu kwa tofauti ya pointi tano. Kuna pointi tatu hapo za kucheza wenyewe kwa wenyewe na Man City na wao. Watakupokutana itakuwa zimebaki mechi tano.

“Kama Arsenal itafungwa na Man City, na hapo mechi zitakuwa zimebaki tano presha itakuwa kubwa kwa Arteta na timu yake, kwa sababu hawajawahi kubeba ubingwa kwenye staili ya aina hiyo, wakati wenzao Man City wana uzoefu. Aprili 29 hadi Mei 6, hapo Arsenal ndo itakwenda kupoteza ubingwa.”

Gary Neville naye amesisitiza Man City itachukua ubingwa, akiendelea kushikilia msimamo wake wa kwamba Arsenal haina ubavu wa kubeba taji hilo kwa msimu huu.

Wakati huo huo, staa wa zamani wa Arsenal, Paul Merson anaamini kurejea kwa straika Gabriel Jesus kutamzidishia tu presha Arteta kwenye kupanga kikosi chake juu ya nani aanze na nani akae benchi.

Kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal katika mechi 27 ilizocheza hadi sasa, imeshinda 21, sare tatu na vichapo vitano na hivyo kukusanya pointi 66. Imefunga mabao 62 na kufunga 25, hivyo ina chanya 37 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika kuelekea mechi 11 zilizobaki kwa Arsenal kutimiza malengo yao ya ubingwa wa ligi msimu huu, hivi ndivyo The Gunners itakavyokwenda mechi moja baada ya nyingine katika kulinda pointi zake na kubeba ubingwa.


Jumapili, Machi 19 vs Crystal Palace (Emirates)

Arteta na jeshi lake la Arsenal litatumia fursa muhimu ya kuweka pengo la pointi nane kileleni dhidi ya Man City, wakati itakapokipiga na Crystal Palace uwanjani Emirates. Man City haitakuwa na mechi kwenye ligi kwa wikiendi hiyo. Arsenal na Palace zimekutana mara 27 kwenye ligi na wao wameshinda 15, saba nyumbani na nane ugenini, huku Palace yenyewe ikishinda nne tu, mbili nyumbani na mbili ugenini na mechi nane ziliisha kwa sare. Uzuri Palace inanolewa na nahodha wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira. Itakuwaje? Mechi mbili za mwisho, kila mmoja ameshinda yake aliyokuwa nyumbani.


Jumamosi, Aprili 1 vs Leeds United (Emirates)

Wakati mwingine mzuri wa Arteta na Arsenal yake kuzidi kujitanua kileleni kwenye msimamo wa ligi itakapokuwa nyumbani Emirates kukipiga na Leeds United.

Arsenal na Leeds kwenye ligi zimekutana mara 29 na katika mechi hizo, zimetoka sare mara tano, huku Arsenal ikishinda 16, mara 10 nyumbani na sita ugenini, Leeds ikiwa imeshinda mara nane tu, tano nyumbani na tatu ugenini. Arsenal imeshinda mechi zote nne za mwisho ilizocheza na Leeds United.


Jumapili, Aprili 9 vs Liverpool (Anfield)

Mtihani wa kwanza kwa Arteta utakuwa kuikabili Liverpool uwanjani Anfield. Liverpool na Arsenal zimekutana mara 61 kwenye ligi na Arsenal imeshinda mara 17 tu, 11 ikiwa nyumbani na sita tu ilishinda Anfield, wakati Liverpool imeshinda 25, mara 16 ikiwa nyumbani na tisa ugenini, huku mechi 19 zilikuwa sare. Mechi mbili za mwisho, kila moja imeshinda mara moja, lakini katika mechi tano za mwisho, Arsenal haijawahi kushinda Anfield.


Jumapili, Aprili 16 vs West Ham (London Stadium)

Arsenal imeishinda mara nyingi West Ham kwenye Ligi Kuu England, lakini shida ni kwamba katika mechi tano za mwisho, haijawahi kushinda ugenini kwa West Ham. Kwa ujumla wake, miamba hiyo imekutana mara 53 kwenye ligi, Arsenal ikishinda 35, mara 21 ikiwa nyumbani na 14 ugenini, huku West Ham ikishinda mara nane, tatu nyumbani na tano ugenini na kuna mechi 10 zilimalizika kwa wababe hao wa London derby kugawana pointi. West Ham haipo kwenye ubora, lakini kocha wake David Moyes ni mzoefu kwenye ligi.


Ijumaa, Aprili 21 vs Southampton (Emirates)

Arsenal itarudi Emirates, Aprili 21 kukipiga na Southampton katika mechi nyingine muhimu kusaka pointi za ubingwa. Arsenal imeshinda mara 25 katika mechi 47 za ligi ilizokutana na Southampton, huku 16 ilishinda Emirates na tisa ugenini, St Mary’s, huku wenzao wakishinda mara nane tu na zote nyumbani, ikiwa haijawahi kushinda hata mara moja ugenini. Mechi 14 zilimalizika kwa sare. Lakini, mechi mbili za mwisho – walizokutana miamba hiyo, moja ilimalizika kwa sare na nyingine, Arsenal ilikubali kichapo. Mechi hiyo inatazamiwa kuwa ngumu.


Jumatano, Aprili 26 vs Man City (Etihad)

Wapinzani wawili kwenye mbio za ubingwa watamaliza ubishi Aprili 26 huko uwanjani Emirates. Rekodi za jumla kwenye Ligi Kuu England, Arsenal na Man City zimekutana mara 51, huku Arsenal ikishinda 23, mara 12 nyumbani na 11 ugenini, huku Man City ikishinda 18, mara 11 nyumbani na saba ugenini. Mechi 10 zilimalizika kwa sare.

Lakini, ugumu kwa Arsenal ni kwamba kwenye mechi tano za mwisho alizokutana na Man City imepoteza zote, kikiwamo kichapo cha mabao 5-0.


Jumamosi, Aprili 29 vs Chelsea (Emirates)

Kipute cha London derby. Mechi hii ni mwendelezo wa wiki ngumu kwa Arsenal kutokana na kuwa na ratiba ya kibabe kabisa kwenye ligi. Arsenal na Chelsea zimekutana mara 61 kwenye ligi, huku Arsenal ikishinda 24, mara 14 ikiwa nyumbani na 10 ugenini, huku Chelsea ikishinda mara 20, mechi 13 ikiwa nyumbani na saba ugenini, huku mechi 17 zilimalizika kwa sare. Rekodi ipo upande wa Arsenal, ambapo katika mechi tano za mwisho, imeshinda mara nne ikiwamo mbili za karibuni.


Jumamosi, Mei 6 vs Newcastle (St. James’ Park)

Kiwango cha Newcastle United kwa msimu huu ndicho kitu kinachofanya mchezo wa ligi dhidi ya Arsenal kutabiriwa kuwa mgumu. Mechi mbili za mwisho miamba hiyo ilipokutana, Arsenal imefungwa moja na kutoka sare nyingi, huku kwenye rekodi ya jumla zimekutana mara 55 kwenye ligi na 11 zilimalizika kwa sare.

Arsenal imeshinda 33, mara 21 ikiwa nyumbani na 12 ugenini, wakati Newcastle imeshinda 11, saba ikiwa nyumbani na nne ugenini. Newcastle United inafukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.


Jumamosi, Mei 13 vs Brighton (Emirates)

Brighton na Arsenal zinapokutana, yoyote anafungwa kutokana na rekodi zao zilivyo na hakuna timu inayotamba kuwa ni mbabe wa mwenzake. Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal na Brighton zimekutana mara 11, huku kila moja ikishinda mara nne, tena kwa uwiano sawa, mbili nyumbani na mbili ugenini, huku mechi tatu baina yao zilimalizika kwa sare.

Mechi mbili zilizopita, Arsenal imeshinda moja na Brighton imeshinda nyingine, huku kinachovutia kila moja ikishinda ugenini.


Jumamosi, Mei 20 vs Nottingham Forest (City Ground)

Mara ya mwisho kwa Nottingham Forest kuifunga Arsenal kwenye Ligi Kuu England uwanjani City Ground ilikuwa Desemba 21, 1999 iliposhinda 2-1. Zaidi ya hapo, Arsenal imeshinda tu mechi hizo, ambapo kwenye ligi zimekutana mara 11, imeshinda saba, mara nne nyumbani na tatu ugenini, huku mechi tatu zilimalizika kwa sare na Nottingham Forest ikishinda moja tu nyumbani. Zitakuwa City Ground, zitafanyaje?


Jumapili, Mei 28 vs Wolves (Emirates)

Kama Arsenal itashinda pointi za kibabe na kufika siku ya mwisho ya msimu huu kwenye Ligi Kuu England ikiwa bado kileleni, basi itashingilia ubingwa ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, Emirates itakapokipiga dhidi ya Wolves.

Kwenye ligi, miamba hiyo imekutana mara 17, Arsenal imeshinda 11, nne nyumbani na saba ugenini, huko Wolves ikishinda tatu tu, mbili nyumbani na moja ugenini, huku mechi tatu zilimalizika kwa sare.

Mechi tano za mwisho zilizokutana kwenye ligi, Arsenal imeshinda tatu na Wolves mara mbili.