Liverpool V Arsenal kitaeleweka

Muktasari:
- Liverpool na Arsenal zimekutana mara 60 ambapo Liverpool imeshinda mara 20, zimetoka sare mara 21 huku Arsenal ikipata ushindi mara 19.
LONDON, ENGLAND: Wakati Ligi Kuu ya England inaelekea ukingoni bado kuna vita ya kuwania nafasi nne za juu katika Ligi hiyo ambapo timu mbalimbali zinapambana ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Mchezo mkubwa utakuwa kati ya Mabingwa wapya Liverpool watakao kuwa kwenye Uwanja wa Anfield kuwakaribisha washika mitutu wa Jiji la London, Arsenal.

Liverpool na Arsenal zimekutana mara 60 ambapo Liverpool imeshinda mara 20, zimetoka sare mara 21 huku Arsenal ikipata ushindi mara 19.
Arsenal inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 67 nyuma ya Mabingwa Liverpool wanaoongoza katika msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na jumla ya pointi 82.
Arsenal wanahitaji pointi tatu katika mchezo wa leo ili kuendelea kuhakikisha wanasalia katika nafasi ya pili ambayo inaonekana kukaribiwa na Manchester City inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 65.

Mchezo wa mapema utawakutanisha Newcastle United dhidi ya Chelsea saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa St James’ Park. Huu utakuwa ni mchezo wenye ushindani wa aina yake kwani timu zote mbili zinalingana pointi zikiwa na 63 huku Necastle ikiwa nafasi ya nne kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Mchezo mwingine utafanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford ambapo Manchester United itakuwa na kibarua cha kuikabili West Ham United. Man United inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 39 huku West Ham ikishika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 37.

Michezo mingine itakayochezwa leo EPL itawakutanisha Nottingham Forest itakayokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa City Ground dhidi ya Leicester City. Crystal Palace itakuwa ugenini kukabiliana na Tottenham.