Wanachukua Kombe

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola ameshangilia kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutamba – sasa twendeni tukabebe mataji matatu.
Chama lake Guardiola, Manchester City limeichapa Real Madrid 4-0 uwanjani Etihad katika nusu fainali ya pili na kutinga fainali kwa jumla ya mabao 5-1 na sasa watakipiga na Inter Milan katika mchezo wa fainali utakaofanyika Instanbul.
Na sasa imebakiza ushindi kwenye mechi tatu kufikia mafanikio yaliyowahi kufikiwa na mahasimu wao Manchester United ilipobeba mataji matatu 1999 ubingwa wa Ligi Kuu England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na Guardiola alisema: “Tumefikia sasa pale ambapo wachezaji wanaweza kufikiria hilo, kuna mwenekano. Bado mechi tatu mbele. Moja katika kila michuano. Tunaweza.
“Tunahitaji ushindi mmoja tu kwenye Ligi Kuu England, kisha ushindi dhidi ya majirani zetu kwenye Kombe la FA na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya timu ya Italia.
“Ni furaha kufika fainali na tutakwenda kucheza na Inter Milan na tutakwenda kufurahia mchezo huo.”

Miaka mitatu iliyopita, Man City ilichapwa kwenye fainali mjini Porto walipopigwa bao 1-0 na Chelsea. Lakini, kwa sasa ushindi dhidi ya Chelsea uwanjani Etihad, Jumapili utawafanya wabebe taji la tatu la Ligi Kuu England mfululizo na taji la tano katika misimu sita ya Guardiola katika kikosi hicho.
Baada ya hapo watakipiga na Man United kwenye fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley, Juni 3. Na baada ya hapo itakwenda kuwakabili Inter mjini Istanbul, Uturuki kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wikiendi inayofuatia.
Guardiola alisema: “Tunahitaji kumalizana na Ligi Kuu England haraka iwezekanavyo na kisha tutajiandaa na mchezo wa Manchester United na Inter Milan.

“Tuna mechi moja moja tu zimebaki kwenye kubabe mataji yote hayo matatu na sasa tumefika fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya na nusu fainali moja katika kipindi cha misimu mitatu. Kiwango cha timu ni cha aina yake. Ni ngumu sana katika zama za sasa kufanya hiki ambacho timu imekuwa ikifanya.”
Ushindi huo dhidi ya Real Madrid ulimfanya Guardiola kocha aliyeshinda mechi 100 kwa haraka zaidi kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na alisema ushindi huo ni kulipa kisasi cha msimu uliopita wakati walipochapwa na Wahispaniola hao katika hatua kama hiyo ya nusu fainali.

“Mchezo unakupa nafasi ya kulipa kisasi na tumekuwa na bahati ya kutosha kutumia fursa hiyo. Niliona wazi timu ilikuwa tayari kwa mapambano na tumefanya kwa kiwango," alisema Guardiola.

Bernardo Silva alifunga mara mbili katika usiku wenye kumbukumbu za kutosha kwenye michuano ya Ulaya na alisema: “Ulikuwa usiku safi kwetu. Ni hisia isiyoelezeka kufika fainali tena, matumaini tutashinda msimu huu.”
Baada ya sare ya 1-1 uwanjani Bernabeu, Man City iliwakabili Real Madrid, waliokuwa mabingwa watetezi kwa umakini mkubwa kwenye mechi ya Etihad na kufunga mara mbili kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Silva.

Bao la kujifunga la Eder Militao liliwaongezea faida Man City kwenye kipindi cha pili kabla ya Julian Alvarez kufunga bao la nne kwenye muda wa majeruhi.
Bernardo alisema: “Kiwango changu kwenye mechi ya Madrid hakikuwa vile nilitaka, nilitaka kufidia kwa sababu sikucheza vizuri mechi ya kwanza. Nilihitaji kufanya vizuri kwa ajili ya wachzaji wenzangu, mashabiki na nilijaribu kufanya nilivyofanya, nimefurahi sana.”
Matokeo hayo kwa Madrid hayakuwa ambayo Carlo Ancelotti ametaka katika kusherehekea kuwa kocha aliyecheza mechi nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya 191, moja juu ya Sir Alex Ferguson.

Na Ancelotti alisema: “Tulicheza dhidi ya wapinzani ambao walistahili kushinda, walicheza kwa nguvu, kwa ubora na walitumia nafasi zao. Walikuwa bora zaidi yetu, tulikuwa bora mwaka jana. Unapoingia nusu fainali unakutana na timu ambayo ni nzuri, waliokwenye ubora, utapoteza tu mechi.”
Kipigo hicho kinaacha sintofahamu kubwa kwenye mustakabali wa kocha Ancelotti huko Real Madrid kutokana na La Liga kubebwa na Barcelona na Ligi ya Mabingwa Ulaya kukomea hatua ya nusu fainali na mwenyewe alisema: “Rais amekuwa kimya kwa wiki mbili zilizopita, hakuna mashaka juu ya kubaki kwangu.”