Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wamepika nafasi kibao ligi za Ulaya msimu 2017/18

Muktasari:

Kwenye jambo hilo ndipo wanapopatikana wachezaji waliofunga mabao mengi, waliopiga asisti nyingi, waliopiga pasi nyingi, waliookoa hatari nyingi na hata wale walionyeshwa kadi nyingi iwe za njano au nyekundu.

LONDON, ENGLAND. MISIMU ya Ligi Kuu za Ulaya inapomalizika, basi kitu kinachobaki kutazamwa ni mchango wa kila mchezaji kwenye vikosi vya ligi hizo.

Kwenye jambo hilo ndipo wanapopatikana wachezaji waliofunga mabao mengi, waliopiga asisti nyingi, waliopiga pasi nyingi, waliookoa hatari nyingi na hata wale walionyeshwa kadi nyingi iwe za njano au nyekundu.

Kwenye hilo hilo kunapatikana pia wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi za mashambulizi kwa timu zao kufunga mabao muhimu yaliyowafanya kushinda mechi zao.

Hii hapa orodha ya wachezaji walioongoza kwa kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi kwenye ligi mbalimbali za Ulaya msimu huu, huku Dimitri Payet akiwafunika wote.

13. Alexis Sanchez

- nafasi 77

Staa wa Chile, Alexis Sanchez, amekuwa akidaiwa kushuka kiwango baada ya kufunga mabao machache msimu huu kwenye vikosi vyote Arsenal na Manchester United alikokwenda kujiunga katika dirisha la Januari. Lakini, kwenye Ligi Kuu England, Sanchez alikosa mechi saba, lakini bado amefanikiwa kuingia kwenye orodha ya wakali waliotengeneza nafasi nyingi za mashambulizi kwa msimu huu, akifanya hivyo mara 77. Wachezaji wengine waliotengeneza nafasi kama hizo ni Xherdan Shaqiri huko Stoke City na Lucas Perez, anayefanya mambo yake Deportivo La Coruna alikokwenda kwa mkopo akitokea Arsenal.

12. Aleksandar Kolarov

- nafasi 78

Manchester City ilimuona kama vile ameishiwa ujuzi na hana makali tena na kuamua kumuondoa kwenye kikosi chake, lakini mambo yamekuwa tofauti tangu beki huyo wa kushoto alipotua katika kikosi cha AS Roma. Kwa msimu huu kwenye Serie A, staa huyo wa Serbia alipiga asisti nane kikosini Roma, huku akitengeneza pia nafasi 78 za mashambulizi kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya Ulaya ambapo walitupwa nje kwenye hatua ya nusu fainali na Liverpool.

11. Suso

- nafasi 79

Kama kuna sababu kubwa iliyoifanya AC Milan kuwa na walau msimu mzuri kwenye Serie A basi ni kuwapo kwa huduma ya mchezaji Suso.

Staa huyo wa zamani wa Liverpool amekuwa kwenye kiwango bora kabisa na kuwa fundi mitambo wa mashambulizi ya AC Milan kwenye Seria A msimu huu, mahali ambapo amepiga asisti saba. Kuhusu nafasi za mashambulizi, staa huyo amepika nafasi 79, sawa na alivyofanya Philipp Max huko kwenye Bundesliga na kufanya jina lake kuingia kwenye kikosi cha Ujerumani kitakachokwenda fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

10. Malcom

- nafasi 82

Jina lake limekuwa gumzo kwelikweli huko England hasa ukizingatia anasakwa na vigogo wa ligi hiyo, Liverpool na Arsenal zikitaka huduma yake. Malcom amekuwa na msimu mzuri kwelikweli kwenye kikosi cha Bordeaux kinachoshiriki Ligi Kuu England na kasi yake ya ndani ya mchezo ndicho kitu ambacho kimezifanya Liverpool na Arsenal kupiga hesabu za kumsajili.

Bado ana umri mdogo kwani kwa sasa ana miaka 21 tu, lakini shughuli yake ya ndani ya uwanja ni pevu, akiwa ametengeneza nafasi 82 za mashambulizi. Mchezaji mwingine aliyetengeneza nafasi kama hizo ni Pascal Gross wa Brighton.

9. Eden Hazard

- nafasi 84

Jina lake limekuwa likitajwa sana na kuwekwa kwenye orodha ya wakali ambao huenda Real Madrid ikatumia pesa kuwasajili kwenye dirisha lijalo la usajili. Staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, anayekipiga kwenye kikosi cha Chelsea, ni mmoja kati ya wachezaji wenye viwango vya ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu England, ukizingatia pia uwezo wake wa kupasia nyavu. Kwa msimu huu, Chelsea ilichokuwa imekikosa ni mchezaji tu mahiri wa kutupia wavuni kwa sababu wapishi walikuwapo, akiwamo Hazard, ambaye alitengeneza nafasi 84 za mashambulizi.

Staa mwingine wa klabu ya Ulaya, aliyetengeneza nafasi kama hizo ni Mathieu Dossevi wa Standard Liege ya Ubelgiji.

8. Lionel Messi

- nafasi 86

Hakuna kitu ambacho Lionel Messi hawezi kukifanya ndani ya uwanja wa soka. Kuna wakati huko mazoezini alijaribu kucheza hata nafasi ya kipa na alionyesha makali yake.

Akiwa kinara wa mabao kwenye La Liga, bila ya shaka staa huyo wa Barcelona amethibitisha ufundi wake wa kuwatesa makipa wa upinzani na hivyo kufunga mabao 34 na kuasisti mara 12.

Kwa msimu huu, Messi ametengeneza nafasi 86 za mashambulizi kuhakikisha Barcelona inakuwa bize kwenye kupiga hodi kwenye goli la wapinzani muda wote kwenye mechi zake ilizocheza. Barcelona ndio mabingwa wa La Liga msimu huu.

7. Mesut Ozil

- nafasi 89

Staa wa Arsenal, Mesut Ozil anazidi kuwagawa watu kwenye makundi mawili. Wapo wale wanaomini staa huyo uwezo wake ni mkubwa na anastahili kubaki Arsenal, lakini kuna lile kundi jingine linaloamini mchezaji huyo hana maajabu yoyote, akiondoka ni sawa tu. Lakini, yote kwa yote, Ozil atabaki kuwa mchezaji wa kiwango cha juu na ndiyo maana mchango wake umekuwa mkubwa ambapo kwenye kikosi cha Arsenal, akiwa ametengeneza nafasi 89 za mashambulizi na kupiga asisti nane na kufunga mabao manne kwa msimu uliomalizika hivi karibuni.

Mchezaji mwingine aliyetengeneza nafasi kama hizo ni Luis Alberto wa Lazio, ambaye pia amepiga asisti 14 na kufunga mabao 11.

6. Cesc Fabregas

- nafasi 93

Moja kati ya vipaji matata kabisa kwenye Ligi Kuu England na ndiyo maana amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu yake anayocheza huko Chelsea. Kwa wakali waliotisha kwa kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi katika ligi za msimu huu huko Ulaya, Mhispaniola huyo ni miongoni mwao baada ya kutengeneza nafasi 93. Kwa Fabregas hilo jambo la kutengeneza nafasi za mashambulizi ni kama kawaida yake tu. Mchezaji mwingine aliyepiga nafasi kama hizo ni Alejandro Gomez wa Atalanta ya Italia na Benjamin Bourigeaud wa Rennes.

4. Christian Eriksen

- nafasi 95

Supastaa wa Denmark, Christian Eriksen alicheza soka la kiwango cha juu msimu uliomalizika hivi karibuni huko Tottenham Hotspur.

Kwenye mechi alizocheza akiwa na kikosi hicho, Eriksen ametengeneza nafasi 95 za mashambulizi. Staa huyo amekuwa na jicho la pasi na mara nyingi pasi zake pia zimekuwa sahihi, ambapo ndiye aliyekuwa hatari kwa kumtengenezea nafasi Harry Kane na mwenzake Dele Alli kufunga mabao tu kwenye Ligi Kuu England kuisaidia timu yao kumaliza ligi ndani ya Top Four.

3. Lorenzo Insigne

- nafasi 95

Fowadi wa Napoli, Lorenzo Insigne ametengeneza nafasi 95 za mashambulizi na kuongoza kwenye Serie A, akiwa mchezaji aliyefanya hivyo mara nyingi zaidi kwenye ligi hiyo. Lakini, makali yake hayo yamekuwa si mali kitu kwa sababu timu yake imeshindwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo ambao umenyakuliwa tena na Juventus.

Hata hivyo, Insigne atabaki kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Napoli kutokana na mchango wake.

2. Kevin De Bruyne

- nafasi 106

Staa wa Kibelgiji, Kevin De Bruyne, alikuwa jiwe la dhahabu kwenye kikosi cha Manchester City kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliomalizika hivi karibuni.

Katika ligi hiyo, De Bruyne alitengeneza nafasi 106 za mashambulizi na kuwa mchezaji aliyefanya hivyo mara nyingi zaidi kwenye ligi hiyo. Katika nafasi hizo 106 za mashambulizi alizotengeneza, KDB alipiga asisti 16 na kubeba tuzo.

1.Dimitri Payet

- nafasi 121

Pengine kitu ambacho staa wa Ufaransa, Dimitri Payet, anajutia kwa sasa ni kuumia katika kipindi hiki ambacho zimebaki wiki chache kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Staa huyo aliumia kwenye mechi ya fainali ya Europa League, ambapo kikosi chake cha Olympique Marseille kilikubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Atletico Madrid.

Payet ametengeneza nafasi nyingi sana za mashambuli msimu huu, akifanya hivyo mara 121, huku akipiga pia asisti 20 katika michuano yote aliyoitumikia Marseille.