Waliofuzu, wanaopewa nafasi ya kubeba Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kwenye nchi za Canada, Mexico na Marekani. England imefuzu fainali hizo kibabe, ilishinda mechi zote nane kwenye Kundi K na haijaruhusu bao lolote na hivyo kufuzu fainali za nane mfululizo za michuano hiyo.
LONDON, ENGLAND: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zinahesabu miezi tu kabla ya kuanza rasmi, huku zikiwa zimebaki timu sita tu ili kupata idadi kamili ya miamba itakayochuana kwenye kusaka ubingwa huo wa dunia.
Fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kwenye nchi za Canada, Mexico na Marekani. England imefuzu fainali hizo kibabe, ilishinda mechi zote nane kwenye Kundi K na haijaruhusu bao lolote na hivyo kufuzu fainali za nane mfululizo za michuano hiyo.
Kutokana na timu mwenyeji kuwa tatu, hivyo Marekani, Canada na Mexico, zenyewe zimefuzu na zinasubiri tu mchakamchaka uanze. Japan ilikuwa nchi ya kwanza isiyokuwa mwenyeji kufuzu fainali hizo za Fifa.
Mabingwa watetezi Argentina na mabingwa mara tano Brazil watakuwapo, wakati Jordan na Uzbekistan ni kati tu ya nchi zitakazocheza fainali za dunia kwa mara ya kwanza.
Timu gani zilizofuzu Kombe la Dunia 2026?
WENYEJI: Canada, Mexico na Marekani.
AFC: Australia, Iran, Japan, Jordan, Qatar, Saudi Arabia, Korea Kusini, Uzbekistan.
CAF: Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia.
CONCACAF: Panama, Curacao, Haiti.
CONMEBOL: Argentina, Brazil, Colombia, Ecuador, Paraguay, Uruguay.
OFC: New Zealand
UEFA: Ujerumani, Uswisi, Scotland, Ufaransa, Hispania, Ureno, Uholanzi, Austria, Norway, Ubelgiji, England, Croatia.
MCHUJO: Kuna timu sita zitafuzu kupitia mchujo ili kukamilisha timu zote zitakazoshiriki.
Timu gani inapewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa?
Wacheza kamari wameshaanza ubashiri wao wa kutambua ni timu gani inayopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa fainali hizo za Kombe la Dunia 2026.
Kwenye mchakato huo, zimetajwa timu tano, ambazo zinapewa nafasi ya kuibuka mabingwa kwenye ubingwa huo wa dunia.
5. ARGENTINA; Mabingwa watetezi wametajwa kwenye namba tano katika orodha ya timu zinazoweza kubeba taji la Kombe la Dunia 2026, huku mashabiki wakifahamu wazi mara chache zilizowahi kutokea kwa bingwa mtetezi kubeba taji mara ya pili mfululizo.
Ni Italia tu (1934/1938) na Brazil ya Pele (1958-1962) ndizo zilizowahi kutetea ubingwa huo wa Kombe la Dunia. Ubingwa wa Argentina 2022 uliigomea Ufaransa kutetea taji hilo ililobeba 2018 baada ya kuwachapa kwenye mchezo wa fainali.
4. BRAZIL; Timu iliyobeba ubingwa wa dunia mara nyingi zaidi nayo imewekwa kwenye orodha, ikitajwa kwenye namba nne, hicho chama hilo linalonolewa na Carlo Ancelotti litakuwa na kazi nzito kulirudisha taifa hilo kwenye ubabe wake.
Mtaliano huyo atakuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuifundisha Brazil kwenye mechi za kiushindani tangu mwaka 1925.
Ancelotti ameshuhudia akishinda mara tatu, sare moja na vipigo viwili kwenye mechi za kimataifa. Rekodi zinaonyesha hakuna kocha wa kigeni aliyewahi kushinda Kombe la Dunia, hivyo Ancelotti ana kazi nzito ya kwenda kuvunja rekodi hiyo.
3. UFARANSA; Les Bleus imefika fainali mara nne katika fainali saba zilizopita za Kombe la Dunia na ilishindwa kwa penalti kufikia rekodi yake ya kutetea taji hilo la ubingwa wa dunia huko Qatar.
Kylian Mbappe, aliyefunga hat-trick kwenye fainali hiyo iliyopita kwa sasa ndiye nahodha wa Ufaransa na amekuwa kwenye kiwango bora sana huko Real Madrid.
Kingine kuhusu Ufaransa ni kwamba ina wachezaji wengi mahiri, akiwamo Michael Olise na Ousmane Dembele wanaomfanya kocha Didier Deschamps kuwa na uhakika wa kwenda kufanya jambo huko Amerika Kaskazini.
2. ENGLAND; Kama ilivyo kwa Brazil, England yenyewe pia iligeukia kwa kocha wa kigeni katika kuelekea fainali hizo za Kombe la Dunia 2026.
Kama mechi za kufuzu zilikuwa nyepesi kwa kocha Thomas Tuchel, England inaamini inaweza kwenda kufanya vyema kwenye fainali hizo za dunia.
England inajiamini kuwa na kikosi kilichosheheni ya mastaa wengi wa maana akiwamo straika, Harry Kane, ambaye ni nahodha wa timu hiyo kwa sasa, ikiamini itakwenda Kombe la Dunia kujaribu kushinda tena ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu 1966.
1. HISPANIA; Timu ambayo iliichapa England kwenye fainali ya Euro 2024 kwa sasa ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia, ikiaminika inaweza kwenda kurudia makali ya mwaka 2008 hadi 2010.
Kabla ya kuichapa England, Hispania ilianza kuzichapa Italia, Ujerumani na Ufaransa kuonyesha kwamba ni timu iliyopo kwenye ubora mkubwa.
Hispania ilifika pia fainali ya Nations League mwaka huu, ikaenda kupoteza kwa mikwaju ya penalti mbele ya Ureno.
Hispania ina mastaa wa maana, akiwamo Pedri, Lamine Yamal, Fabian Ruiz na Dani Olmo kwa kuwataja kwa uchache, ambao wana vipaji vya hali ya juu.
Tarehe za kijanja Kombe la Dunia 2026
Msimu wa Ligi Kuu England 2025/26 utafika tamati Jumapili ya Mei 24, wakati fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itapigwa Jumamosi, Mei 30. Baada ya hapo, Kombe la Dunia 2026, litaanza Alhamisi, Juni 11, na fainali yake itapigwa Jumapili, Julai 19.
FIFA imepanga michuano hiyo itafanyika kwa siku 57, ambapo kutakuwa na siku 16 za maandalizi na siku 39 za michuano yote. Fainali hizo zitakuwa na makundi 12 zenye timu nne nne, ambapo zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kila kundi zitafuzu hatua inayofuatia, pamoja na zile nane zilizomamaliza nafasi ya tatu bora zitaingia raundi ya 32.
Kutakuwa mechi kila siku kuanzia Juni 11 hadi Julai 7, kisha kutakuwa na mapumziko ya Julai 8 kabla ya kuingia hatua ya robo fainali. Nusu fainali zitafanyika Julai 14 na Julai 15, wakati mechi ya mshindi wa tatu itapigwa Julai 18, siku moja kabla ya kupigwa fainali yenyewe.