DR Congo ina dua zetu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Sasa jamaa zetu wanapigania kurudi kwa mara ya pili katika Fainali za Kombe la Dunia na wameingia katika hatua ya mwisho ya mchujo itakayofanyika Machi mwakani kusaka nafasi mbili za kushiriki fainali hizo za mwaka 2026 zitaandaliwa na Marekani, Canada na Mexico.
MAJIRANI zetu DR Congo mara ya mwisho walishiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1974 zilipofanyika Ujerumani ambako waliishia hatua ya makundi ambayo walifungwa mechi zote tatu dhidi ya Yugoslavia, Brazil na Scotland.
Sasa jamaa zetu wanapigania kurudi kwa mara ya pili katika Fainali za Kombe la Dunia na wameingia katika hatua ya mwisho ya mchujo itakayofanyika Machi mwakani kusaka nafasi mbili za kushiriki fainali hizo za mwaka 2026 zitaandaliwa na Marekani, Canada na Mexico.
Haijaingia hatua hiyo kwa kubahatisha kwani imepata ushindi dhidi ya vigogo viwili vya soka Afrika, Cameroon na Nigeria katika hatua ya kwanza ya mchujo kwa upande wa bara hili.
Kwa pamoja hapa kijiweni tumekubaliana tuiombee DR Congo ifanye vizuri katika hatua ya mwisho ya mchujo na ipate tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia na tumeamua hivyo kwa sababu mbili za msingi.
Kwanza ni mahusiano mazuri ambayo Tanzania na DR Congo tumekuwa nayo kwa muda mrefu. Nchi hizi mbili na raia wake tumekuwa tukishirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa pato la Tanzania ni DR Congo kupitia uingizaji wa mizigo yake pale katika Bandari ya Dar es Salaam na kisha kusafirishwa kupelekwa nchini mwao.
Sababu ya pili ni mchango ambao DR Congo imekuwa ikiutoa kwa soka letu. Kwa muda mrefu, klabu za Tanzania zimekuwa zikichukua wachezaji kutoka timu za DR Congo na kwa hakika wengi wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri na kuzisaidia klabu zetu.
Mfano kwa sasa hivi tunao akina Maxi Nzengeli, Elie Mpanzu, Japhte Kitambala, Nelson Munganga, David Mwanakibuta, Heritier Makambo, Chadrack Boka na Horso Mwaku ni baadhi ya nyota wa DR Congo wanaofanya vyema katika ligi yetu.
Tusisahau katika kikosi cha DR Congo hivi sasa kuna Fiston Mayele ambaye japo hayupo Ligi Kuu Bara kwa sasa, anaitangaza vyema kwa vile aling’aa alipokuwa nchini akiitumikia Yanga.
Chochote anachokifanya Mayele, bado Watanzania wanakifuatilia kama wanavyomfuatilia sasa akiisaka tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia 2026 iwapo Les Leopards itatoboa play-off.