Walid Regragui: Haikuwa rahisi kuifunga Comoro, tumejifunza kitu
Muktasari:
- Regragui ameeleza kuwa, ni jambo la kawaida kwa timu kukutana na changamoto katika mechi ya kwanza kutokana na presha, matarajio makubwa na hitaji la kuzoea mazingira ya mashindano.
Kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui, amesema mechi ya ufunguzi ya AFCON 2025 dhidi ya Comoro haikuwa rahisi kwa kikosi chake, lakini amefurahishwa na namna wachezaji walivyobadilika na kuonyesha kiwango bora katika kipindi cha pili.
Regragui ameeleza kuwa, ni jambo la kawaida kwa timu kukutana na changamoto katika mechi ya kwanza kutokana na presha, matarajio makubwa na hitaji la kuzoea mazingira ya mashindano.
Amesema wachezaji wa kikosi chake walionekana kuwa na wasiwasi katika kipindi cha kwanza, hali iliyosababisha mechi kuwa ngumu zaidi kuliko walivyotarajia.
“Hii ilikuwa mechi ya kwanza na huwa ni mgumu kila mara. Tulihitaji muda wa kuingia katika mechi na kujiamini. Lakini kipindi cha pili tulibadilika, tukacheza kwa umakini zaidi, tukatawala mchezo na kuonyesha uwezo halisi wa timu yetu.” amesema Regragui.
Kocha huyo pia amesifu nidhamu na ari ya wachezaji wake, akisema walifuata maelekezo aliyowapa wakati wa mapumziko na kuboresha mbinu zao, hasa katika eneo la kiungo na ushambuliaji, huku akiongeza kuwa mabadiliko aliyoyafanya yalisaidia kuongeza kasi na ubora wa mechi.
Regragui pia amewataka mashabiki wa Morocco kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, akisisitiza kuwa bado kuna mechi nyingi mbele na timu ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri zaidi kadri mashindano yanavyoendelea.
“Tuna mengi ya kujifunza kupitia mechi yetu na Comoro, lakini muhimu ni kwamba tulipata matokeo na kuonyesha tabia ya kupambana. Hii ni hatua ya mwanzo tu,” amehitimisha kocha huyo.
Bao la kwanza la Morocco lilifungwa na Brahim Díaz katika dakika ya 55, baada ya kumalizia vizuri mpira uliokuwa umeachwa ndani ya eneo la hatari. Bao la pili lilifungwa na Ayoub El Kaabi katika dakika ya 74, muda mfupi baada ya kuingia uwanjani, akionyesha ubora wake katika safu ya ushambuliaji.
Ushindi huo unaifanya Morocco kuongoza msimamo wa Kundi A baada ya mechi ya kwanza, ikiwa na pointi tatu na tofauti ya mabao mawili ya kufunga. Matokeo hayo yanaipa timu hiyo mwanzo mzuri na nafasi nzuri ya kujiweka katika mazingira chanya ya kufuzu hatua inayofuata, huku ikiongeza kujiamini kuelekea mechi zinazofuata kwenye kundi hilo.