Prime
Ushindi Yanga, Azam upo hapa
SAHAU kilichotokea Mwanza saa 70, zilizopita leo ni hadithi mpya kabisa kwa kocha Abdihamid Moallin wa Yanga anajua hatma ya ubingwa ipo mikononi wa Florent Ibenge wa Azam kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kocha Moallin alishuhudia Yanga ikipokwa ubingwa wa Kombe la CRDB baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Azam, ndani ya siku moja anapata nafasi ya kujiuliza upya mbele ya Ibenge anayeonaka kuwa na wakati mzuri baada ya kuzifunga robo tatu ya timu zote alizopata nazo sare katika mzunguko wa kwanza.
Yanga na Azam zinakutana takribani saa 70 na dakika 30 tu za kupumzika na kujiandaa kabla ya kukutana tena kwenye mchezo huo, hiyo ni chini ya siku tatu kamili za mapumziko baada ya mechi ya dakika 120.
Tofauti na mechi ya Kirumba iliyokuwa ikitafuta tiketi ya fainali, safari hii kuna pointi tatu ambazo zinaweza kubadili kabisa ramani ya mbio za ubingwa na nafasi za juu za msimamo wa ligi.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kinara wa ligi na pointi 66 huku Simba nafasi ya pili na pointi 64 na Azam yenye pointi 58 nayo bado ina malengo ya kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kabla ya mwisho wa msimu.
Lakini baada ya dakika 120 za Kirumba, kila benchi la ufundi lina kazi kubwa ya kufanya, ili kurejea na mbinu mpya mechi ya ligi.
MIPIRA YA JUU IMEWAUMIZA YANGA
Jambo la kwanza ambalo Yanga lazima ilifanyie kazi ni namna ya kuzuia mipira ya juu, mabao yote walifungwa kwa mtindo mmoja.
Katika mchezo uliopita, Azam ilionyesha kuwa haitegemei pasi fupifupi pekee kujenga mashambulizi, Ibenge alitengeneza mpango wa kutumia nguvu za Jean Ngita ambaye alitawala kwa kiasi kikubwa mipira ya juu dhidi ya mabeki wa Yanga.
Ngita hakufunga, lakini mchango wake ulionekana wazi kwenye bao la kwanza ambapo alimdondoshea mpira Himid Mao aliyefunga kwa kichwa.
Katika nyakati nyingi za mchezo huo, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca' walijikuta wakipambana siyo tu na mshambuliaji huyo bali pia na mipira ya pili iliyokuwa ikiokotwa na viungo wa Azam.
Ukitazama bao la pili pia lilifungwa kwa kichwa na beki Lameck Lawi na hata bao la tatu chanzo ilikuwa mpira wa juu ambao aliufunga Jephte Kitambala baada ya Bacca kumrudishia mpira kipa Diarra, nyota huyo wa Azam aliuunga juu kwa juu na kufunga.
Kama Azam itaendelea kutumia mfumo huo, Yanga italazimika kuhakikisha kiungo wake wa ulinzi unakuwa karibu na mabeki wa kati ili kukusanya mipira yote inayorudi baada ya Ngita au Kitambala kushinda mipira hiyo ya juu wote hao ni washambuliaji warefu.
DEPU NA DUBE NI SILAHA?
Mabadiliko ya Yanga kipindi cha pili
baada ya Depu kuingia na kusimama karibu na Prince Dube, safu ya ulinzi ya Azam ilianza kupata shida.
Awali, Twalib Mohamed na Yoro Diaby walikuwa wakicheza kwa uhuru wakikabiliana na mshambuliaji mmoja.
Lakini mara baada ya Yanga kuongeza mtu mwingine kwenye eneo la ushambuliaji, mabeki hao walilazimika kugawana majukumu na hapo ndipo mianya ilianza kuonekana.
Kutokana na hali hiyo, Yanga inaweza kufikiria kuanza mechi ijayo ikiwa na washambuliaji wawili au angalau kuwa na mpango wa mapema wa kuongeza nguvu ndani ya boksi.
OKELLO APATE MPIRA ZAIDI
Allan Okello ni mmoja wa wachezaji ambao wanaweza kuamua mechi na takwimu zake zinamtambulisha kama mmoja wa wachezaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Yanga akiwa na mabao 11 na asisti saba.
Azam ilifanikiwa kupunguza nafasi za Okello kwa kumweka chini ya presha ya Himid Mao na Yahya Zayd.
Iwapo Yanga itataka kutawala mchezo wa leo, lazima Okello apate uhuru zaidi wa kucheza kati ya safu za Azam, hapo ndipo atakapoweza kuwatengenezea nafasi Prince Dube, Depu, Pacome na Max Nzengeli.
AZAM ISIPOTEZE NIDHAMU
Kwa upande wa Azam, ushindi wa Kirumba umeleta furaha, pia umeacha fundisho kubwa.
Kadi nyekundu ya Yoro Diaby karibu iliharibu kila kitu, mpaka dakika ya 69, Azam ilikuwa inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuimaliza mechi.
Baada ya kubaki na wachezaji 10, ililazimika kutumia nguvu nyingi kujilinda na kwa kiasi kikubwa ikapoteza umiliki wa mpira.
Katika mechi ya ligi ambayo Yanga itakuwa chini ya presha ya kutafuta ushindi, makosa kama hayo yanaweza kugharimu matokeo.
Ibenge atalazimika kuhakikisha mabeki wake wanakuwa watulivu zaidi hasa wanapokabiliwa na washambuliaji wenye kasi kama Prince Dube.
FEISAL NDIYE UFUNGUO
Kama kuna mchezaji ambaye anaweza kuamua hatma ya Azam katika mchezo huo basi ni Feisal Salum mwenye mabao 14na asisti nane.
Katika kipindi cha kwanza alipata nafasi ya kugeuka na kutazama mbele, Azam ilionekana kuwa timu yenye hatari kubwa.
Lakini Yanga ilipoanza kutawala eneo la kati, Feisal alianza kupotea taratibu,
Ibenge atalazimika kutafuta njia ya kumpa nafasi zaidi ya kucheza karibu na eneo la mwisho.
Feisal akiwa kwenye ubora wake, Azam huwa na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi hata bila kumiliki mpira kwa muda mrefu.
VITA KUBWA ITAKUWA VIUNGO
Ingawa Ngita, Kitambala, Dube na Dube wanaweza kuwa na kazi kubwa ya kuongoza safu za ushambuliaji ya timu hizo, ukweli ni kwamba mechi inaweza kuamuliwa katikati ya uwanja.
Duke Abuya, Mudathir Yahya na Allan Okello kwa upande wa Yanga watakutana na Himid Mao, Yahya Zayd na Feisal Salum wa Azam katika vita ya kutawala mpira.
Timu itakayoshinda eneo hilo ndiyo itakayokuwa na nafasi kubwa ya kuamua mwelekeo wa mchezo.
Katika uwanja wa Kirumba, Yanga ilianza vibaya lakini ikaimarika kipindi cha pili, Azam ilianza vizuri lakini ikamaliza mechi ikijilinda kwa muda mrefu.
Hivyo kila kocha ana maswali ya kujibu kabla ya pambano la Zanzibar.
SAUTI ZA MAKOCHA
Kocha wa Azam, Ibenge amesema ushindi wa Kombe la CRDB haujafunga hesabu zake dhidi ya Yanga.
"Tumeshinda na tumefuzu fainali, lakini bado tuna mechi nyingine dhidi ya Yanga, Hatuna muda wa kusherehekea, tunapaswa kurikava na kujiandaa," alisema kocha huyo.
Kwa upande wa Yanga, Kaimu Kocha Mkuu Abdihamid Moallin amesema timu yake itaendelea kupambana katika mechi zilizobaki za ligi.
"Tumepoteza nafasi ya kucheza fainali lakini bado tuna malengo yetu kwenye ligi, lazima tujipange vizuri kwa mchezo unaofuata," alisema.