Wafanyakazi Man United wanyimwa tiketi

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Daily Mail, United imekataa kutoa tiketi za bure kwa wafanyakazi wake kwa mechi ya fainali ya Europa League itakayofanyika Bilbao.
MANCHESTER, ENGLAND: VIGOGO wa Manchester United wamekataa kutoa tiketi za bure kwa wafanyakazi wa klabu kwa ajili ya fainali ya Europa League ikiwa ni juhudi za tajiri wa timu hiyo Sir Jim Ratcliffe za kupunguza gharama.
Kwa mujibu wa Daily Mail, United imekataa kutoa tiketi za bure kwa wafanyakazi wake kwa mechi ya fainali ya Europa League itakayofanyika Bilbao.
Klabu zote mbili Manchester United na Tottenham zitakazokutana kwenye fainali hiyo, zimetengewa tiketi 15,000 kila moja, lakini Man United imeamua kuuza tiketi zote ilizopewa kwa mashabiki wao.
Badala ya kugawa tiketi, Man United inapanga kufanya hafla ya kutazama mechi hiyo kwa pamoja kwa ajili ya wafanyakazi, na wataruhusiwa kuwaleta wageni wao.
Hata hivyo, klabu hiyo itatoa vinywaji viwili tu vya bure kwa kila mfanyakazi aliyeteuliwa, huku wageni wao wakitakiwa kulipia huduma.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa, utaratibu uko tofauti kwa Tottenham ambayo itatoa tiketi moja ya bure kwa kila mmoja wa wafanyakazi wao 700, ingawa bado haijulikani ni wangapi wataitumia nafasi hiyo, kutokana na gharama kubwa za kusafiri kwenda Bilbao na bei za hoteli.
Man United inaripotiwa kusisitiza kuwa kipaumbele ni mashabiki wa klabu, ndio maana imeamua tiketi nyingi ziende kwa mashabiki wanaokwenda uwanjani kuliko kwa wafanyakazi.
Hatua hii inaelezwa kuwa sehemu ya mpango wa kupunguza gharama unaoendelezwa na mmiliki wa sehemu ya hisa za timu hiyo Ratcliffe.