Desabre amkumbuka Wan-Bissaka, kuzikabili Mali na Madagascar

Muktasari:
- Wan-Bissaka, ambaye alizaliwa London, England lana asili ya DR Congo kupitia wazazi wake na ameonyesha dhamira ya kuwakilisha taifa la asili yake baada ya kusubiri kwa muda mrefu nafasi ya kuitwa England bila mafanikio.
Aliyekuwa beki wa Manchester United na sasa West Ham United, Aaron Wan-Bissaka, ameitwa rasmi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) kwa ajili ya mechi mbili za kimataifa dhidi ya Mali na Madagascar.
Wan-Bissaka, ambaye alizaliwa London, England lana asili ya DR Congo kupitia wazazi wake na ameonyesha dhamira ya kuwakilisha taifa la asili yake baada ya kusubiri kwa muda mrefu nafasi ya kuitwa England bila mafanikio.
Huu unaweza kuwa uamuzi mzuri kwa DR Congo, wakati ambao wanaongoza kundi lao la kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia la 2026.
Kocha Mkuu wa DR Congo, Sébastien Desabre, amesema ujio wa Wan-Bissaka utaongeza uimara katika safu ya ulinzi na kusaidia kuimarisha kikosi kuelekea mashindano yajayo.
“Tunamkaribisha Aaron kwa mikono miwili. Ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu England na tunaamini atakuwa msaada mkubwa kwa timu yetu,” amesema Desabre.
Wan-Bissaka (26), amecheza mechi zaidi ya 100 akiwa na Manchester United na amesifika kwa uwezo wake wa kuzuia, nidhamu uwanjani, na kasi ya kushambulia kutoka upande wa kulia.
Wan-Bissaka aliwahi kuchezea timu za vijana za England za umri chini ya miaka 20 na chini ya miaka 21 lakini hajawahi kuchezea kikosi cha wakubwa cha Three Lions, jambo lililomruhusu kujiunga na DR Congo.