Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bao Francesco Acerbi linavyohusishwa na 'kuzimu'

Muktasari:

  • Hii ni mechi ya mkondo wa pili baada ya ile ya mkondo wa kwanza kumalizika kwa sare ya 3-3 dimbani Camp Nou, nyumbani kwa Barcelona.

Ulikuwa ni usiku babu kubwa katika dimba la Giuseppe Meazza ambalo pia huitwa San Siro, nyumbani kwa Inter Milan.

Ulikuwa ni usiku wa kukamilisha nusu fainali babu kubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kati ya Inter Milan na FC Barcelona.

Hii ni mechi ya mkondo wa pili baada ya ile ya mkondo wa kwanza kumalizika kwa sare ya 3-3 dimbani Camp Nou, nyumbani kwa Barcelona.

Saa inasoma ni dakika ya 92:40 na ubao wa matokeo unasoma Inter 2-3 Barcelona.

Ni ajabu sana kwa sababu wenyeji Inter Milan walianza kwa kuongoza 2-0 hadi mapumziko na sasa zikiwa zimesalia sekunde chache mchezo kuisha, ubao umegeuka.

Barcelona wanaelekea kufuzu fainali kwa maumivu ya Inter Milan walioko uwanja wa nyumbani.

Ndipo ikafika ile sekunde ya 40 ya dakika ya 90+2 ambayo ndiyo sababu ya makala hii ya leo.

Hii ni makala iliyobeba moja ya simulizi zenye kusisimua sana siyo kwa sababu ya kutolewa kwa Barcelona, bali kwa sababu inahadithia simulizi ya maisha ya binadamu.

Ni simulizi ya mlinzi wa kati wa Inter Milan mwenye miaka 37 - Francesco Acerbi - aliyesawazisha bao na kuwakumbusha Barcelona kwamba haikuwa kwa bahati mbaya Inter Milan kucheza nusu fainali yao ya pili ndani ya miaka mitatu.

HAKUPASWA KABISA KUWEPO PALE

Sahau kwanza kuhusu yeye kama mlinzi wa kati kuwepo eneo lile la ushambuliaji. Halafu jiulize, 'alikuwa anafanya nini dimbani pale anacheza nusu fainali ya ligi ya mabingwa akiwa na miaka 37?

Mwaka 2012, Francesco Acerbi alikuwa akiwakiwa na nyota njema ya asubuhi jua lake la soka lilikuwa linachomoza.

Alisaini mkataba mnono na AC Milan (baada ya msimu mmoja tu wa Serie A akiwa na Chievo)...mambo yanaanza kumuendea sawa.

Lakini ghafla jua lake la mafanikio lililoanza kupamzazuka, likagubikwa na wingu zito pale baba yake mzazi alipofariki dunia.

Hii ilimuumiza sana. "Baada ya baba kufariki, wakati anachezea AC Milan, kiwango chake kiliporomoka sana," alinukuliwa na gazeti la La Repubblica.

"Ikawa ni kama nilisahau kucheza, au kwanini nacheza. Nikaanza kulewa, na niamini mimi, nilikunywa kila kitu."

Kiwango kikashuka na AC Milan wakamtoa kwa mkopo kwenda Sassuolo.

Akiwa hapo akagundulika kuwa na saratani ya tezi dume, majanga juu ya majanga.

Miezi michache baadaye akafanyiwa upasuaji kuondoa tatizo lake akajaribu kurudi uwanjani, lakini wapi, ugonjwa ukamrudia tena na safari hii kwa ukatili zaidi, ikabidi apigwe mionzi.

Maisha yakabadilika, badala ya kupambania makombe uwanjani, Acerbi akaanza kupambania maisha yake hospitali.

"Ni ajabu na kweli, lakini saratani ndiyo iliniokoa. Nadhani kuupata ule ugonjwa kulinikuza mimi kama binadamu."

Ilimchukua zaidi ya miaka miwili, kabla ya kupona kabisa na kurudi uwanjani lakini hata hivyo, hakuna klabu iliyomtaka.

Akarudi Sassuolo kuanza upya kuifukuzia ndoto yake ya kucheza soka iliyokaribia kuporwa na msiba wa baba, ulevi sugu na baadaye saratani.

Akiwa na miaka 30 akaivutia Lazio na kusaini nao mkataba. Mkataba huu aliupokea kwa hisia kali kama mchezaji wa kutoka akademi anavyosaini mkataba wake wa kwanza.

Akiwa na miaka 34, akasaini mkataba wa Inter Milan, hebu ona.

Yaani ile njia ambayo hupita wachezaji chipukizi, yeye aliipita akiwa katika umri wa miaka ya 30.

Mtu aliyepata mpongo wa mawazo baada ya kufiwa na baba yaka mzazi, akatumbukia katika uraibu wa pombe na baadaye kugundulika kuwa na saratani.

Huyu ni kama mtu aliyeishi mara mbili, yaani aliishi, akanusa kuzimu halafu akarudi tena duniani na kufunga bao muhimu liliokoa maisha ya Inter Milan katika ligi ya mabingwa.

Na kubwa kuliko yote, hilo ni bao lake la kwanza katika maisha yake ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Ukiliangalia bao lake, unaweza kusema yeye kama mlinzi wa kati hakupaswa kuwepo eneo lile ambalo ni la mshambuliaji wa kati lakini alikuwepo.

Na ukiangalia historia ya maisha yake, utaona kabisa hakupaswa kuwepo dimbani siku ile akiwa na miaka 37 lakini alikuwepo, Mungu akamsimamia, akatimiza ndoto yake.