Mipira ya kurusha na maajabu yake
Muktasari:
- Kwa ujumla idadi ya mipira ya kurusha ya kawaida imepungua katika Kombe la Dunia 2026, lakini ile mirefu (long throws) na mabao yatokanayo na mipira ya kurusha yanaongezeka.
MEXICO CITY, MEXICO: WAKATI ikiwa ni siku ya tatu ya mechi za mtoano za hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026, ulimwengu wa soka umeshuhudia mabadiliko kibao katika soka ambayo yamegeuka mjadala katika vijiwe vya mashabiki ikiwamo timu kutochelewesha kuanzisha mpira na mchezaji anayepaswa kutoka uwanjani kufanya hivyo haraka.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea fainali hizo zimezaa mjadala mwingine ukiangazia mipira ya kurusha (throw-ins) inayodaiwa sasa kuwa balaa jingine katika kuzibeba timu na kuziathiri zingine zinaposhindwa kujipanga ipasavyo.
Kwa ujumla idadi ya mipira ya kurusha ya kawaida imepungua katika Kombe la Dunia 2026, lakini ile mirefu (long throws) na mabao yatokanayo na mipira ya kurusha yanaongezeka. Tuanze na takwimu. Iwe ni mipira mirefu au mifupi inaathiri kwa kiasi kikubwa mechi na kama ulifuatilia kwa karibu Ligi Kuu England msimu uliopita mipira mirefu ya kurusha imerudi kwa kasi.
Kama ulidhani ingewekwa pembeni kwenye Kombe la Dunia, umekosea. Haijakuwa na ushawishi mkubwa kama ilivyokuwa Ligi Kuu England 2025-26, lakini zinaonekana sana Amerika Kaskazini katika mashindano yanayoendelea ikitumika kwa ufanisi mkubwa.
Kutokana na mipira hiyo kuna mabao sita yaliyotokana na ‘throw-ins’ kwenye Kombe la Dunia 2026, ikiwa ni sawa na jumla ya ile iliyorushwa katika mashindano ya 2010, 2014, 2018 na 2022 kwa pamoja. Pia kulikuwa na mabao mawili katika kila moja ya mashindano matatu ya kwanza, huku 2022 kukiwa hakuna bao hata moja.
Vilevile mabao mawili yaliyofungwa na Czechia katika mashindano ya mwaka huu ambao tayari wameondolewa, ambapo Ladislav Krejeí alifunga kwa kichwa kutokana na mipira mirefu ya kurusha ya Vladimír Coufal dhidi ya Korea Kusini, huku Michal Sadílek akifunga dhidi ya Afrika Kusini baada ya mpira kuanza kwa kurushwa upande wa kulia kutoka eneo la katikati ya uwanja.
Katika hatua ya makundi, Tunisia pia walishuhudia mipira yao mirefu ya kurusha ikiingia kwenye eneo la hatari la Sweden ikitolewa, lakini mpira uliorudishwa haraka kwa Omar Rekik akafunga kwa kichwa. Lilikuwa bao lao pekee katika kipigo cha mabao 5-1, ingawa kocha Sabri Lamouchi angefurahishwa na mbinu hiyo japokuwa alifukuzwa kazi siku chache baadaye.
Kisha katika kipindi hicho hicho mabao matatu kutokana na mipira ya kurusha katika siku moja wiki iliyopita yalipatikana. Bao la Leroy Sané wa Ujerumani dhidi ya Ecuador lilitokana na mpira wa aina hiyo kutoka kwa David Raum kwenda Florian Wirtz aliyempasia winga wa Galatasaray akafunga ndani ya dakika mbili.
Baada ya hapo mabao mawili zaidi yalifuatia katika ushindi wa Uturuki wa 3-2 dhidi ya Marekani. Wenyeji walifunga 2-2 kupitia Mark McKenzie baada ya mipira mirefu kusafishwa vibaya, kisha Sebastian Berhalter akafunga. Hata hivyo Uturuki walishinda kwa mpira wa haraka uliomalizikia kwa Kaan Ayhan kufunga.
Mabao sita kutokana na mipira ya kurusha hivi sasa ni ya pili kwa wingi katika historia ya Kombe la Dunia tangu 1966, sawa na 2002 na 1994.
Katika mipira mirefu ya kurusha inayoelekezwa ndani ya boksi (angalau mita 20), Canada ilikuwa timu iliyoitumia zaidi katika hatua ya makundi ikifanya hivyo mara 20 ndani ya boksi la wapinzani, karibu mara mbili ya New Zealand 12. Pia iliongeza mingine mitano dhidi ya Afrika Kusini katika hatua ya 32 bora. Czechia wamekuwa bora zaidi kwa ufanisi wakiwa na minane iliyosababisha mashuti.
Kwa ujumla, kumekuwapo na mipira mirefu ya kurusha 39 kabla ya mechi zilizochezwa leo usiku iliyosababisha mashuti katika Kombe hili la Dunia. Mwaka 2022 ilikuwa 12, 2018 (19), 2014 (10), 2010 (25) na 2006 (17).
Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo, mabao bado ni matatu tu yaliyotokana moja kwa moja na mipira ya kurusha, jambo linaloonyesha ufanisi wake bado mdogo. Licha ya hilo, ni zaidi kuliko kawaida, hasa ukizingatia hakuna mashindano yaliyopita yaliyofikisha zaidi ya mabao mawili kutokana na aina hii ya mipira.
Kumekuwapo na mipira mirefu 177 iliyoelekezwa ndani ya boksi katika mechi 73, wastani ukiwa 2.4 kwa mchezo. Linganisha na 2022 na 2018 ambapo ilikuwa 1.6, na 2014 ikiwa 1.3. Mwaka 2010 ilikuwa 2.3 na 2006 ikiwa 1.9, ambapo Tunisia pekee ndiyo haikujaribu.
Hata hivyo mipira ya kurusha kwa ujumla imepungua, wastani 36.8 kwa mchezo. Tangu mwanzoni mwa karne hii, hakujawahi kuwa chini ya 40. Mwaka 2010 ilikuwa 50.1.
FIFA ilitangaza sheria mpya kwamba kama mwamuzi ataona ucheleweshaji, hesabu ya sekunde tano itaonyeshwa, vinginevyo mpira hutolewa kwa timu pinzani. Wastani wa muda umeshuka hadi sekunde 13.0 kutoka 14.8 (2018) na 15.7 (2022), jambo linaloonyesha kasi mpya ya mchezo.
Je, kasi hii inasaidia mashambulizi? Inaweza kuwafanya timu kutumia throw-ins kama nafasi ya kushambulia badala ya kupoteza muda na kuwashangaza mabeki.
Huenda timu zinaona kama nafasi ya faida ndogo muhimu katika mashindano ya mtoano. Mwenendo huu unaweza kuendelea, na wachezaji kufikiria mara mbili kabla ya kuruhusu mpira utoke nje kama njia salama ya kujilinda.