Wababe waliocheza nusu fainali nyingi Ulaya

Muktasari:

WAKATI michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ipo kwenye hatua ya nusu fainali, kuna rekodi nyingi ambazo zinatarajiwa kuwekwa msimu huu.

LONDON, ENGLAND. WAKATI michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ipo kwenye hatua ya nusu fainali, kuna rekodi nyingi ambazo zinatarajiwa kuwekwa msimu huu.

Miongoni mwa rekodi hizo ni wachezaji kucheza mechi nyingi za hatua ya hiyo. Wakati Mbappe, Neymar na mastaa wengine wakiifukuzia rekodi hiyo, kuna baadhi ya wachezaji wameshaifikia. Mbali ya kucheza michezo mingi, pia wamevaa medali za ushindi kwa kunyakua taji la michuano hiyo.

Mwanaspoti linakuletea wachezaji watano waliocheza mechi nyingi Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Thomas Muller,

Bayern Munchen

Sergio Ramos

Real Madrid

Mechi:15

Kuna wachezaji wawili wamefungana kwa kuche-za me-chi 15. Sergio Ramos amechukua mataji manne wakati Muller akichukua mawili.Katika michezo 15, Ramos yote akiwa na Real Madrid sawa na Muller yote akiwa na Bayern Munich.

Muller alianza kuichezea Bayern kwenye timu za vijana kabla ya kupandishwa 2009, lakini Ramos alitua 2005 akitokea Sevilla.


Lionel Messi

Timu Barcelona

Mechi:15

Fundi mwingine ambaye maisha yake ameyatoa sadaka kwa ajili ya Barcelona. Messi amechukua mataji manne akiwa na Barca akicheza michezo 15 ya nusu fainali.

Mbali ya rekodi hiyo pia anashika nafasi ya pili kuwa mfungaji bora wa muda wote akifunga mabao 120. Kwa sasa mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na stori kubwa imekuwa ni kitendawili cha timu gani atajiunga nayo baada ya kuachana na wababe hao.


Xavier Hernandez

Timu:Barcelona

Mechi:16

Asilimia kubwa ya maisha yake ya soka aliyatumia akiwa na Barcelona aliyoichezea kuanzia timu za vijana hadi ya wakubwa.

Akiwa na Barca alifanikiwa

kutwaa mataji manne ya michuano hiyo na alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika safu ya kiungo. Kwa ujumla amecheza mechi 16 za nusu fainali na zote akiwa na Barcelona.

Aliondoka Camp Nou mwaka 2015 na kutua Al-Sadd SC ambako alicheza hadi 2019, kisha akastaafu na kukabidhiwa mikoba ya kuwa kocha mkuu.


Xabi Alonso

Timu: Liverpool, Real Madrid, Bayern Munich

Mechi;17

Staa huyu amecheza nusu fainali 17, lakini amechukua makombe mawili tu - moja akiwa na Liverpool na lingine na Real Madrid.

Akiwa na Liverpool alifanikiwa kucheza nusu fainali sita na zote ilikuwa dhidi ya Chelsea. Alipojiunga na Real Madrid aliicheza mechi nane na mwisho akamalizia Bayern Munich kucheza mechi nne,


Cristiano Ronaldo

Timu: Manchester United, Real Madrid

Mechi: 21

Katika orodha hii Ronaldo anaongoza kwa kuchukua taji hilo mara nyingi. Mbali ya kulichukua mara nyingi, Ronaldo ndiye mchezaji pekee anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi za nusu fainali akicheza 21.

Nusu fainali hizo amecheza akiwa na timu ya Manchester United ambako alianzia kuandika historia ya kuchukua taji hilo kwa mara ya kwanza msimu wa 2007/2008 walipoifunga Chelsea kwa mikwaju ya penalti kwenye mchezo wa fainali. Mataji mengine manne aliyachukua akiwa na Real Madrid. Kwa sasa yupo Juventus.