Waarabu washuka kwa Kepa Arrizabalaga

Muktasari:
- Kipa huyu amewaambia mabosi wa Chelsea anahitaji muda kabla ya kukutana na kocha mpya Enzo Maresca na kutoa uamuzi wake wa mwisho juu ya hatma yake.
TOVUTI ya Marca imeripoti kipa wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Real Madrid ana ofa nono ya kujiunga na Al Ittihad ya Saudi Arabia katika dirisha hili.
Kipa huyu amewaambia mabosi wa Chelsea anahitaji muda kabla ya kukutana na kocha mpya Enzo Maresca na kutoa uamuzi wake wa mwisho juu ya hatma yake.
Kepa aliondoka Chelsea kwa sababu hakuwa anapata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo hata kama atarejea anataka kuhakikishiwa namba kwanza.
Chelsea ipo tayari kumbakisha lakini kama atalazimisha kuondoka inataka kumuuza mazima na sio kwa mkopo kama msimu uliopita.
Ikiwa atajiunga na Ittihad kipa huyu anaweza kupata mshahara unaofikia Pauni 600,000 kwa wiki ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya mshahara wake wa sasa.
Mbali ya ofa ya Saudia, Madrid pia inafikiria kumsainisha mkataba wa kudumu baada ya kuvutiwa na kiwango chake. Mkataba wake unamalizika mwaka 2025.
Wakati huo huo Arsenal na Manchester United zinadaiwa kuwa katika vita ya kuiwania saini ya beki wa Crystal Palace, Marc Guehi, 23, ambaye ameonyesha wazi anataka kuondoka katika dirisha hili licha ya Palace kutaka kumpa ofa ya kusaini mkataba mpya. Mkataba wake wa sasa na Palace unamalizika mwaka 2026. Msimu uliopita alicheza mechi 29 za michuano yote na kuonyesha kiwango kizuri.
IPSWICH ina matumaini makubwa ya kuwapata wachezaji wawili wa Hull City ambao ni winga Jaden Philogene, 22, na beki Jacob Greaves, 23, dirisha hili na wamepanga kutoa Pauni 35 milioni kwa mastaa hao wote. Ipswich ambayo imapanda daraja kucheza Ligi Kuu England msimu ujao katika vita ya kuiwania huduma ya mastaa hawa inapambana na timu nyingine za England kama Everton.
TOTTENHAM inataka kutoa pesa na mchezaji ili kuipata huduma ya kiungo wa Aston Villa, Jacob Ramsey, 23, katika dirisha hili. Taarifa kutoka Skysports zinaeleza kwamba Spurs inataka kumtumia kiungo wao Giovani lo Celso, 28, kama sehemu ya ofa ya kuipata huduma ya Ramsey ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
CHELSEA imefikia makubaliano na Atlanta United ili kumnunua beki wa kushoto wa timu hiyo, Caleb Wiley, 19, kwa Pauni 8.5 milioni dirisha hili, ingawa haitomwingiza katika kikosi chao moja kwa moja na badala yake itamtoa kwa mkopo kwenda Strasbourg. Msimu uliopita Wiley alicheza mechi 22 za michuano yote. Mkataba wake unamalizika mwaka 2025.
LEEDS ina matumaini ya kuingiza zaidi ya Pauni 70 milioni dirisha hili kwa kuwauza mastaa watatu wa timu yao, winga Mholanzi, Crysencio Summerville, 22, na washambuliaji Georginio Rutter, 22, kutoka Ufaransa na Wilfried Gnonto, 20, wa Italia. Mastaa hao wanawindwa na timu nyingi na Leeds inataka kutumia pesa itakazopata kutokana na kuwauza kusajili wengine.
BAYERN Munich ipo tayari kuuza wachezaji wake sita wanaohusishwa na timu mbalimbali Ulaya dirisha hili ikiwa pamoja na winga Mfaransa, Kingsley Coman, 28, beki wa Uholanzi, Matthijs de Ligt, 24, viungo Wajerumani, Leon Goretzka, 29, Joshua Kimmich, 29, na Serge Gnabry, 28, pamoja na beki wa kushoto Alphonso Davies, 23. Mastaa hawa wote wanawindwa na timu mbalimbali barani Ulaya.
BEKI kisiki wa Nice na Ufaransa, Jean-Clair Todibo, 24, anataka kujiunga na Juventus katika dirisha hili baada ya dili lake la kutua Manchester United kufeli.
Mazungumzo kwa sasa yanaendelea baina ya wawakilishi wake na mabosi wa Juve lakini hakuna mwafaka uliofikiwa. Mkataba wa Todibo unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.