Vozinha avuna kijiji Instagram akifunguka sababu kuangua kilio
Muktasari:
- Mbali na kuzuia mashambulizi ya Hispania kwa dakika 90, kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 pia aliandika historia nje ya uwanja baada ya kupata zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye mtandao wa Instagram ndani ya saa chache baada ya mchezo huo uliopigwa Atlanta, Marekani.
ATLANTA, MAREKANI: KIPA mkongwe wa Cape Verde, Vozinha, ameibuka shujaa wa Kombe la Dunia 2026 baada ya kuiongoza nchi yake kupata suluhu dhidi ya Hispania katika mechi ya kwanza kabisa ya taifa hilo kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Mbali na kuzuia mashambulizi ya Hispania kwa dakika 90, kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 pia aliandika historia nje ya uwanja baada ya kupata zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye mtandao wa Instagram ndani ya saa chache baada ya mchezo huo uliopigwa Atlanta, Marekani.
Vozinha alikuwa nyota wa mechi hiyo baada ya kufanya kuokoa michomo saba muhimu na kuinyima Hispania mabao katika mchezo ambao wengi walitarajia Cape Verde ingeangukia pigo kubwa dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa dunia.
baada ya kipindi cha kwanza kumalizika, wachambuzi wa kituo cha televisheni cha Brazil, Caze TV, walivutiwa na kiwango chake na kuwataka watazamaji kumfuata kwenye Instagram ili kumpongeza kwa alichokuwa akikifanya uwanjani.
Wito huo ulipokelewa kwa kasi ya ajabu ambapo ndani ya dakika chache idadi ya wafuasi wake iliongezeka kutoka chini ya 50,000 hadi zaidi ya 220,000.
Kadri mchezo ulivyoendelea, ndivyo umaarufu wake ulivyozidi kuongezeka. Kufikia dakika ya 60 alikuwa tayari amefikisha zaidi ya wafuasi 350,000 huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kila dakika.
Baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, Vozinha alikuwa amefikisha takribani wafuasi 389,000, lakini ndani ya dakika tano tu idadi hiyo iliongezeka kwa zaidi ya nusu milioni.
Alipofika vyumbani baada ya mechi, kipa huyo alikuwa tayari amevuka alama ya wafuasi milioni moja, jambo lililomshangaza yeye mwenyewe.
Katika mahojiano baada ya mchezo, Vozinha alioneshwa simu iliyokuwa ikionyesha idadi hiyo mpya ya wafuasi na kushindwa kuficha mshangao wake.
"Kabla ya mechi nilikuwa na karibu wafuasi 50,000. Hii ni kitu cha ajabu sana," alisema kwa mshangao.
Aliongeza: "Asanteni sana. Wabrazil wamekuwa wakituonyesha upendo mkubwa siku zote. Tumeuhisi wakati wa safari yetu ya kufuzu na sasa tunaendelea kuuona."
Mbali na mafanikio hayo ya mtandaoni, kipa huyo pia aligusa hisia za wengi alipofunguka kuhusu maisha yake binafsi baada ya mchezo huo.
Vozinha alisema alibubujikwa na machozi baada ya filimbi ya mwisho kwa sababu alikumbuka babu na bibi yake waliomlea tangu akiwa mtoto lakini hawakuweza kushuhudia siku hiyo ya kihistoria kutokana na kufariki dunia miaka michache iliyopita.
Alieleza pia kuwa mama yake alishindwa kusafiri kwenda Marekani kumuunga mkono kutokana na changamoto za kupata viza kwa wakati.
"Niliangua kilio baada ya mchezo. Nililelewa na babu na bibi yangu na walikuwa sehemu kubwa ya maisha yangu. Wangefurahi sana kuona siku hii lakini hawapo tena," alisema.
Sare hiyo imeendelea kutajwa kama moja ya matokeo makubwa ya kushtua katika hatua za mwanzo za Kombe la Dunia 2026, huku Cape Verde ikionesha kuwa haijafika kwenye mashindano hayo kwa bahati mbaya.
Kwa Vozinha, mechi hiyo ilikuwa ya 89 akiwa na timu ya taifa ya Cape Verde tangu aanze kuitumikia mwaka 2012 lakini huenda ikabaki kuwa usiku muhimu zaidi katika maisha yake ya soka.
Kutoka kuwa kipa wa klabu ya Chaves inayocheza daraja la pili nchini Ureno hadi kuwa gumzo la duniani ndani ya saa chache, Vozinha ameonyesha kuwa Kombe la Dunia bado lina uwezo wa kuandika historia zinazobadili maisha ya wachezaji kwa muda mfupi.