Vozinha anatua kwa Messi
Picha kwa msaada wa AI
Muktasari:
- Vozinha mwenye umri wa miaka 40 alijijengea jina kubwa katika mashindano hayo kutokana na kiwango chake cha juu langoni, huku akivutia mamilioni ya mashabiki duniani na kufikisha zaidi ya wafuasi milioni 28.5 kwenye mtandao wake wa Instagram.
LOS ANGELES, MAREKANI: KIPA mkongwe wa Cape Verde, Vozinha, ambaye alikuwa mmoja wa mastaa waliotikisa Kombe la Dunia, anatajwa kuwa mbioni kutua Inter Miami kwa uhamisho wa bure baada ya kumvutia mmiliki wa klabu hiyo, David Beckham.
Vozinha mwenye umri wa miaka 40 alijijengea jina kubwa katika mashindano hayo kutokana na kiwango chake cha juu langoni, huku akivutia mamilioni ya mashabiki duniani na kufikisha zaidi ya wafuasi milioni 28.5 kwenye mtandao wake wa Instagram.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la AS la Hispania, Beckham alivutiwa na uwezo wa kipa huyo baada ya kushuhudia alivyowatesa nyota wa Argentina katika mchezo wa hatua ya 32 Bora, ambapo Cape Verde iliwalazimisha mabingwa hao kwenda dakika za nyongeza kabla ya kuondolewa.
Iwapo dili hilo litakamilika, Vozinha atajiunga na nyota wakubwa duniani akiwemo Lionel Messi, ambaye aliiongoza Argentina kuiondoa Cape Verde, pamoja na Luis Suarez katika kikosi cha Inter Miami.
Safari ya Cape Verde kwenye Kombe la Dunia ilikuwa ya kushangaza baada ya kutoka sare dhidi ya Hispania na Uruguay katika hatua ya makundi kabla ya kuonyesha upinzani mkubwa dhidi ya Argentina ikiwa ni mara ya kwanza wanashiriki michuano hiyo mikubwa.
Umaarufu wa Vozinha uliendelea kuongezeka kutokana na kiwango chake bora, huku hata akitajwa kukamilisha chenga nyingi zaidi katika mechi moja kuliko alizokuwa nazo Cristiano Ronaldo katika hatua hiyo ya mashindano.
Kipa huyo alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kuiwezesha Cape Verde kutoka sare bila kufungana dhidi ya Hispania, huku wengi wakiamini alistahili pia tuzo hiyo dhidi ya Argentina, lakini ikaenda kwa Messi.
Baada ya mchezo huo, Vozinha alisimulia mazungumzo yake na Messi.
“Nilimfuata Messi baada ya mechi. Alinikumbatia na kuniambia, ‘Wewe ni kipa mkubwa. Watu wako wanapaswa kujivunia’. Hayo yalikuwa maneno makubwa sana kwangu,” amesema Vozinha.
“Kusikia maneno kama hayo kutoka kwa Leo Messi kunamaanisha mengi. Nilimshukuru na kumwambia, ‘Asante Leo, wewe ndiye bora zaidi’. Kisha nikamuomba tubadilishane jezi, naye akaniambia angenipa kwenye njia ya kuelekea vyumbani baada ya mahojiano.”
Katika mechi dhidi ya Hispania, Vozinha aliokoa mipira saba ya hatari, huku akifanya sevu nane dhidi ya Argentina na kuwa mwiba kwa washambuliaji wa timu hizo.
Baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora dhidi ya Hispania, Vozinha alionekana akilia kwa hisia kali.
Alieleza kuwa machozi hayo yalitokana na kumbukumbu za babu na bibi yake waliomlea tangu utotoni, ambao walifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.
“Nilikulia kwa babu na bibi zangu. Kwa bahati mbaya hawakuwepo kushuhudia wakati huu kwa sababu walifariki miaka michache iliyopita. Walikuwa kila kitu katika maisha yangu,” amesema. Kipa huyo aliyetumikia timu tano kwa sasa anaichezea Chaves ya mchini Ureno.