Vitendo vya Carvajal, Lamine vyamchukiza De Jong
Muktasari:
- Carvajal mwenye miaka 33, alionekana akionyesha ishara ya kuzungumza sana mbele ya Lamine Yamal, akimaanisha kinda huyo alizungumza maneno mengi ya kuikejeli Real Madrid kabla ya mpambano huo kupigwa Santiago Bernabeu, mjini Madrid.
Kiungo wa Barcelona Frenkie de Jong amemkosoa beki wa pembeni wa Real Madrid, Dani Carvajal, kufuatia kitendo chake cha kumchokoza Lamine Yamal, baada ya mechi ya El Clasico jana Jumapili, Oktoba 26, 2025.
Carvajal mwenye miaka 33, alionekana akionyesha ishara ya kuzungumza sana mbele ya Lamine Yamal, akimaanisha kinda huyo alizungumza maneno mengi ya kuikejeli Real Madrid kabla ya mpambano huo kupigwa Santiago Bernabeu, mjini Madrid.
De Jong amesema Carvajal hakuwa na uharaka wa kumuonyesha kitendo hicho Lamine hadharani, kwani alikuwa na nafasi ya kufanya hivyo wakiwa wawili pekee yao, na kama ingeshindikana angempigia simu na kumwambia.
Amesema kilichotokea baina ya wawili hao na kusababisha fujo baina ya wachezaji wa Barcelona na Real Madrid hakikuwa kitendo kizuri kwa ustawi wa soka la Hispania, ambalo mara nyingi huitazama mechi ya El Clasico kama mfano.
“Kama Carvajal alitaka kuzungumza na Lamine, angeweza kufanya hivyo binafsi, halikuwa jambo zuri kwa watu kama hawa kulumbana hadharani,” amesema De Jong.
“Kama aliona hakupaswa kusema vile, angeweza kumpigia hata simu. Wote ni wachezaji wa Hispania, wanajuana. Kwa nini walifika hatua kama ile, kwangu ulikuwa kama kioja uwanjani?”
Kwa upande mwingine, kiungo wa Real Madrid, Aurélien Tchouaméni amesema maneno ya Yamal hayakuwa ya kuudhi sana, zaidi ya kuwajenga na kuwatamanisha kushinda mechi ya jana.
“Ni maneno tu, hayana nia mbaya. Yalitupa motisha ya kupambana zaidi, lakini kama Lamine anataka kuzungumza, sawa tu, hakuna tatizo,” amesema Tchouaméni.
“Nilipokuwa mdogo nilipenda kuona majibizano kati ya wachezaji wa Barca na Real kabla ya mechi mwishowe, kila kitu kinaamuliwa uwanjani, na anayepoteza mchezo anakubaliana na hilo.”
Kiwango cha Yamal katika mechi ya El Clasico kilikuwa cha chini kuliko kawaida, huku akionekana bado anathiriwa na maumivu ya nyonga.