Vita ya ubingwa EPL ni vuta, nikuvute!
Muktasari:
- Miamba hiyo inachuana jino kwa jino kwenye kuisaka nafasi ya kwanza. Shughuli ni pevu.
LONDON, ENGLAND: MSIMAMO unasoma, pointi nne tu zimetofautisha timu tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Arsenal ipo kileleni ikiwa imekusanya pointi 50 katika mechi 23, ikifuatiwa na Manchester City na Aston Villa zenye pointi 46 kila moja baada ya mechi 23 walizocheza kwenye mikikimikiki hiyo.
Miamba hiyo inachuana jino kwa jino kwenye kuisaka nafasi ya kwanza. Shughuli ni pevu.
Kwenye namba nne ipo Manchester United, iliyokusanya pointi 38 katika mechi 23. Lakini, nafasi ya nne ina vita kali pia, ambapo Chelsea yenye pointi 37 na Liverpool iliyokusanya pointi 36, zinaisaka nafasi hiyo inayotoa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
MAMBO YANAZIDI KUNOGA.
Arsenal ambayo ipo kwenye wasiwasi mkubwa wa kufikiwa na wapinzani wao kileleni kwenye msimamo wa ligi, safari hii imepata nafasi ya kutangulia kucheza ili kuweka pengo la pointi kufikisha saba, wakati itakapokwenda ugenini kukipiga na Leeds United.
Kipute hicho kinapigwa kesho Jumamosi na kwa namna yoyote ile, Mikel Arteta na jeshi lake la Arsenal atahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kuhakikisha wanaongoza ligi bila ya presha bila ya kujali matokeo ya wengine.
Ukiweka kando Arsenal ambayo ushindi wao utaziweka kwenye presha kubwa Man City na Aston Villa kwenye vita hiyo, Chelsea na Liverpool pia zitakuwa kwenye vita kali ya kuwania kushika nafasi ya nne, kuiengua Man United hapo kwa muda, wakati zitakaposhuka uwanjani Jumamosi.
Chelsea itakuwa nyumbani Stamford Bridge kukipiga na wababe wenzao wa London, West Ham United, wakati Liverpool itajimwaga Anfield kuonyesha kazi na Newcastle United. Kwenye karatasi mechi hizo zote ni ngumu. Hivyo, patachimbika.
Mechi nyingine za Jumamosi, Wolves itakuwa nyumbani kukabiliana na Bournemouth, wakati Brighton itakuwa kwenye kasheshe zito la kuwakabili Everton.
Manchester United ambayo kwa sasa inacheza soka la kujipata zaidi tangu ilipoanza kuwa chini ya Kocha Michael Carrick, yenyewe itashuka uwanjani Old Trafford kujaribu kusaka pointi za kuimarisha nafasi yao kwenye Top Four kwa kukabiliana na Fulham, keshokutwa, Jumapili.
Aston Villa na Man City zenyewe zitakuwa zinasikilizia matokeo ya Arsenal ili kuona namna ya kuongeza joto kwenye mbio za ubingwa. Kikosi cha kocha Unai Emery, Aston Villa kitakuwa nyumbani Villa Park kukabiliana na Brentford katika moja ya mechi ngumu kabisa, huku Pep Guardiola na chama lake la Man City litakuwa kwenye kasheshe zito la kuwakabili Tottenham Hotspur ugenini, timu ambayo mara nyingi imekuwa ikimpa wakati mgumu ndani ya uwanja.
Man City inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuzidisha presha katika mbio za ubingwa, lakini Spurs pia ipo kwenye harakati za kujikongoja ili kujiweka pazuri. Mechi nyingine ya Jumapili itakayokuwa ya vuta nikuvute ni ile Nottingham Forest itakapomenyana na Crystal Palace.
Jumatatu kutakuwa na mechi moja tu na Sunderland itakuwa nyumbani Stadium of Light kukipiga na Burnley.