Virgil van Dijk amalizana na Liverpool

Muktasari:
- Awali, Van Dijk ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini baada ya mazungumzo aliyofanya mambo yanaonekana kwenda vizuri na ameshakubali kubakia.
LIVERPOOL, ENGLAND: BAADA ya kufanikisha kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili mshambuliaji wao Mohamed Salah, mabosi wa Liverpool wanadaiwa pia kufikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya beki na kapteni wao, Virgil van Dijk.
Awali, Van Dijk ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini baada ya mazungumzo aliyofanya mambo yanaonekana kwenda vizuri na ameshakubali kubakia.
Staa huyu wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 33 alikuwa akitajwa kuwa kwenye rada za timu za Saudi Arabia zilizokuwa tayari kumpa ofa nono ili akubali kujiunga nao pale mkataba wake utakapomalizika Juni mwaka huu.
Mtaalamu wa masuala ya usajili Fabrizio Romano amefichua kuwa beki huyu atasaini mkataba mpya wa miaka miwili kabla ya mwisho wa msimu huu.
Wiki iliyopita, Van Dijk alidokeza kuwa yuko karibu kusaini mkataba mpya ingawa hakuweka wazi kama ameshafikia makubaliano yoyote.
"Kuna mazungumzo, ndiyo. Sijui yataishaje, tutaona hapo baadaye baada ya kumalizika."
Hii ni habari nyingine kubwa kwa mashabiki wa Liverpool baada ya jana asubuhi timu hiyo kuthibitisha kumsainisha mkataba wa miaka miwili Salah ambaye kwa asilimia kubwa sana ilionekana asingebakia kwani alishawahi hadi kusema hadharani kwamba yupo karibu kuondoka kuliko kubaki.
"Bila shaka nina furaha sana. Tuna kikosi kizuri sasa na hapo zamani, nimesaini kwa sababu naamini tuna nafasi ya kushinda mataji mengine na kufurahia maisha yangu ya mpira, hadi sasa nimekuwa na nyakati nzuri sana hapa, nimeshacheza miaka minane na natumaini itafika 10 baada ya kumaliza mkataba huu mpya, nina furaha sana kwa sababu hapa nimekuwa na miaka yangu bora kabisa kwenye maisha yangu ya soka," alisema Salah jana baada ya kusaini mkataba huo mpya.
Ripoti zinaeleza Salah amesaini mkataba ambao utampa karibia Pauni 400,000 kwa wiki na huenda Van Dijk naye akasaini kwa mkataba unaokaribia sawa na kiasi hicho.
Licha ya kufanikiwa kuwabakisha mastaa hawa wawili, bado Liverpool inaonekana kuwa na asilimia nyingi za kumpoteza beki wao Trent Alexander-Arnold ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu ambapo Real Madrid ndio inapewa nafasi kubwa ya kumchukua.