Vinicius? Lolote linaweza kutokea
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa Brazil, ambaye ana miaka miwili iliyobaki kwenye mkataba wake wa sasa, amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na klabu za Saudi Arabia ambazo zipo tayari kumpa mkwanja wa kutosha.
MADRID, HISPANIA: STAA wa Real Madrid, Vinicius Junior anaweza kuamua kuachana na timu hiyo kama mahitaji ya mshahara anaotaa ili asaini mkataba mpya hayatatekelezwa.
Mchezaji huyo wa Brazil, ambaye ana miaka miwili iliyobaki kwenye mkataba wake wa sasa, amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na klabu za Saudi Arabia ambazo zipo tayari kumpa mkwanja wa kutosha.
Hata hivyo, winga huyo mara zote ambazo timu hizo zimewasilisha ofa za kutaka kumsajili, amekuwa akiwaambia kwamba bado anadhamiria kuendelea kucheza soka la ushindani akiwa katika viunga vya Santiago Bernabeu.
Msimu huu, Vinicius ameanza kwa nguvu ya aina yake akiwa amefunga mabao matatu katika mechi tano alizoichezea timu hiyo.
Madrid imekuwa ikijadiliana na wakala wa Vini kuhusu mkataba mpya tangu mwisho wa mwaka 2024, lakini pande zote mbili bado hazijaweza kufikia makubaliano.
Ripoti zinaonyesha kuwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil alikutana na mabosi wanaomiliki timu za Saudi Arabia Februari mwaka huu ili kusikiliza ofa zao, lakini alizikataa na kufikia Machi, iliripotiwa kuwa alikuwa akikaribia kusaini mkataba mpya na Madrid.
Kwa mujibu wa tovuti ya Diario AS ni kwamba Madrid bado haijafikia mwafaka wowote katika mazungumzo na inadaiwa Vini anataka mshahara sawa na ule ambao Kylian Mbappe anaupata katika klabu hiyo.
Vilevile sababu ya Vini kutaka kuondoka ni kwamba ana wasiwasi kuhusu nafasi yake katika kikosi, kwani anaona inaweza kubadilika chini ya Xabi Alonso ili kumpa uhuru zaidi Mbappe, ingawa kocha huyo Mhispania amesisitiza kuwa Mbrazil huyo ni muhimu katika kikosi chake.