Mvua, radi zatishia mechi ya Uholanzi na Tunisia
Muktasari:
- Mashabiki waliokuwa tayari wameingia ndani ya uwanja walitakiwa kuondoka kwenye maeneo ya wazi na kuelekezwa sehemu salama huku wengine waliokuwa wakifika uwanjani wakizuiliwa ndani ya mabasi katika eneo la maegesho wakisubiri hali ya hewa itulie.
KANSAS CITY, MAREKANI: MECHI ya Kombe la Dunia 2026 inayozikutanisha Uholanzi na Tunisia, ilikuwa katika hatari ya kuahirishwa dakika chache kabla ya kuanza baada ya mamlaka za hali ya hewa kuonya kuhusu uwepo wa mvua kubwa iliyoambatana na radi jijini Kansas.
Mashabiki waliokuwa tayari wameingia ndani ya uwanja walitakiwa kuondoka kwenye maeneo ya wazi na kuelekezwa sehemu salama huku wengine waliokuwa wakifika uwanjani wakizuiliwa ndani ya mabasi katika eneo la maegesho wakisubiri hali ya hewa itulie.
Mawingu mazito yalitanda juu ya uwanja huo huku luninga kubwa za uwanjani zikitoa tahadhari kwa mashabiki.
"Tafadhali ondokeni kwenye maeneo ya wazi na elekeeni sehemu salama ndani ya uwanja kwa kufuata maelekezo ya wahudumu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Tahadhari hiyo ilitolewa baada ya utabiri wa hali ya hewa kuonyesha kuwa kulikuwa na uwezekano wa asilimia 70 wa kutokea kwa mvua kubwa zenye radi katika eneo la Kansas City, hali iliyoongeza hofu ya mafuriko na kuchelewesha mchezo huo muhimu wa Kundi F.
Kwa mujibu wa kanuni za usalama zinazotumika Marekani, mechi yoyote ya wazi haiwezi kuendelea ikiwa radi itagunduliwa ndani ya umbali wa maili nane kutoka uwanjani.
Endapo hali hiyo ingetokea, waamuzi wangekuwa na jukumu la kusimamisha au kuchelewesha mchezo hadi mazingira yatakapokuwa salama.
Hii si mara ya kwanza hali ya hewa kuingilia ratiba ya Kombe la Dunia 2026 kwani wiki hii tayari kulishuhudiwa mchezo wa Ufaransa dhidi ya Iraq kusimama kwa muda kutokana na dhoruba iliyotokea wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza.