Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ecuador yaiduwaza Ujerumani ikifuzu 32 bora Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Kabla ya ushindi wa leo, timu hiyo ilianza kwa kichapo cha bao 1-0, dhidi ya Ivory Coast, kisha mechi yake ya pili kutoka suluhu na Curacao.

NEW JERSEY, MAREKANI: TIMU ya taifa ya Ecuador imehitimisha hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa kwanza katika fainali za mwaka huu, baada ya jana kuiduwaza Ujerumani kwa kuifunga mabao 2-1 na kufuzu hatua ya 32 bora.

Kabla ya ushindi wa leo, timu hiyo ilianza kwa kichapo cha bao 1-0, dhidi ya Ivory Coast, kisha mechi yake ya pili kutoka suluhu na Curacao.

Mechi hiyo ya kundi E, iliyopigwa kwenye Uwanja wa MetLife uliopo katika mji wa East Rutherford, jimbo la New Jersey, Marekani, ilianza kwa Ujerumani kupata bao katika dakika ya pili lililofungwa na winga, Leroy Sane baada ya muunganiko mzuri kati yake na mchezaji mwenzake, Florian Wirtz.

Dakika ya tisa, Ecuador ikasawazisha kupitia kwa Nilson Angulo kwa shuti shuti kali akimalizia kazi nzuri ya Pedro Vite na timu hizo kwenda hadi mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Bao hilo la Angulo ni la kwanza kwa Ecuador katika Kombe la Dunia la mwaka 2026, huku akiwa ni mchezaji wa nne tofauti wa Klabu ya Sunderland ya England kufunga, wakati wachezaji wanaoongoza kwa kupachika mabao mengi hadi sasa ni wa PSG ya Ligi Kuu ya Ufaransa ambao wamefunga sita.

Kipindi cha pili kiliendelea kwa Ujerumani kutawala mechi hiyo, japo ilishtukizwa dakika ya 77, baada ya kufungwa bao la pili na nyota wa Ecuador, Gonzalo Plata aliyemalizia kazi nzuri ya Kevin Rodriguez.

Matokeo hayo yanaifanya Ujerumani kuendelea kubakia kileleni mwa msimamo wa kundi E ikiwa na pointi sita  sawa na Ivory Coast inayoshika nafasi ya pili ila zikitofautiana kwa matokeo ya mchezo baina yao ambao Ujerumani ilishinda huku Ecuador ikiwa ya tatu na pointi nne, wakati Curacao ikiwa na pointi moja ambayo inaifanya kuaga rasmi mashindano.

Ujerumani ni moja ya mataifa yenye mafanikio zaidi duniani katika Kombe la Dunia  kwa kuchukua ubingwa huo mara nne ambazo ni fainali za miaka ya 1954, 1974, 1990 na 2014, huku ikimaliza mshindi wa pili mara nne pia kwa fainali za  1966, 1982, 1986 na 2002.


Pia, Ujerumani imewahi kumaliza mshindi wa tatu mara nne katika Kombe la Dunia katika fainali za 1934, 1970, 2006 na 2010, japo miongoni mwa historia mbovu zaidi kwa taifa hilo ni kutolewa katika hatua ya makundi kwenye fainali za 2018 na 2022.

Miongoni mwa ushindi mkubwa wa kukumbukwa kwa Ujerumani ni wa kuifunga Brazil iliyokuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2014 kwa mabao 7-1, katika hatua ya nusu fainali, ikiwa ni matokeo ya kushangaza zaidi kwenye historia ya Kombe la Dunia.

Kwa upande wa Ecuador imekuwa ni timu inayoimarika taratibu kutoka Bara la Amerika Kusini, ambapo inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tano baada ya kushiriki katika fainali za  2002, 2006, 2014 na 2022.

Katika ushiriki wa Ecuador, mafanikio bora ya timu hiyo ni kwenye fainali za mwaka 2006, zilizofanyika Ujerumani, ambapo ilifika hatua ya 16 bora na kutolewa na England kwa kuchapwa bao 1-0, lililofungwa na David Beckham.

Tofauti na hapo, fainali za 2002, 2014 na 2022 iliishia hatua ya makundi.