Vinicius Jr aibuka shujaa Real Madrid ikiipiga Villarreal
Muktasari:
- Baada ya kipindi cha kwanza kilichojaa huzuni na mashabiki kuwapigia kelele wachezaji wa Real, ilichukua sekunde 90 tu za kipindi cha pili kwa Vinicius kufungua ukurasa wa mabao.
Vinicius Junior amefunga mabao mawili huku Real Madrid ikirejea kwenye njia ya ushindi baada ya kipigo cha fedheha kutoka kwa majirani zao Atletico Madrid wiki iliyopita, kwa kuichapa Villarreal 3-1 Jumamosi Oktoba 4, 2025 na kupanda kileleni mwa La Liga.
Baada ya kipindi cha kwanza kilichojaa huzuni na mashabiki kuwapigia kelele wachezaji wa Real, ilichukua sekunde 90 tu za kipindi cha pili kwa Vinicius kufungua ukurasa wa mabao.
Mshambuliaji huyo wa Kibrazili alipokea mpira wa kichwa uliopigwa na Kylian Mbappe, akapinda kutoka upande wa kushoto na kupiga shuti lililomgonga Santi Comesaña na kumhadaa kipa Arnau Tenas.
Vinicius aliendelea kuwa tishio kwa Villarreal, na katika dakika ya 69 aliongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na Rafa Marín.
Hata hivyo, Villarreal hawakukata tamaa, na muda mfupi baada ya Jude Bellingham kukosa bao akiwa ana kwa ana na kipa, mshambuliaji wa Georgia, Georges Mikautadze, alipiga shuti kali lililompita Thibaut Courtois na kusawazisha.
Bekii wa Villarreal, Santiago Mourino, alionyeshwa kadi ya njano ya pili iliyoambatana na nyekundu baada ya kumvuta Vinicius, na dakika tatu baadaye Mbappé aliihakikishia Real ushindi kwa kufunga bao la tatu akimalizia pasi ya Brahim Díaz.
Hata hivyo, furaha ya ushindi huo ilipungua kidogo baada ya Mbappé kuonekana akichechemea na kuondoka uwanjani akionekana kuumia mguu.
Baada ya mechi hiyo, Real Madrid imefikisha pointi 21 baada ya michezo minane, ikiwa pointi mbili mbele ya Barcelona ambayo itacheza dhidi ya Sevilla, Jumapili Oktoba 5, 2025. Villarreal imesalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 16.
MATOKEO LA LIGA OKTOBA 4, 2025
Oviedo 0-2 Levante
Girona 2-1 Valencia
Athletic Club 2-1 Mallorca
Real Madrid 3-1 Villarreal