Ghafla hadithi ya Vinicius imebadilika
Muktasari:
- Ni ngumu kuamini lakini hilo linatokea sana chini ya kocha Xabi Alonso, mbali ya kumweka benchi katika mchezo huo, tangu kuanza kwa msimu huu mara kadhaa pia Vinicius amekuwa akitolewa katika baadhi ya mechi, anapandwa na hasira lakini atafanya nini, ni basi tu zama zimebadilika, maisha yanakwenda kasi sana.
SIKU kadhaa zilizopita, mtoto wa mzee Jose Paixao, Vinicius Jose Paixao de Oliveira Junior ‘Vinicius Jr’, aliyekuwa akishindania tuzo ya Ballon D’or mwaka jana dhidi ya Rodri, mchezaji aliyekuwa tegemeo wa Real Madrid, mchezaji aliyeonekana kuwa taswira ya Real Madrid alionekana amejikunyata kwa baridi pale kwenye dimba la Estadio Santiago Bernabeu, akianzia benchi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille.
Ni ngumu kuamini lakini hilo linatokea sana chini ya kocha Xabi Alonso, mbali ya kumweka benchi katika mchezo huo, tangu kuanza kwa msimu huu mara kadhaa pia Vinicius amekuwa akitolewa katika baadhi ya mechi, anapandwa na hasira lakini atafanya nini, ni basi tu zama zimebadilika, maisha yanakwenda kasi sana.
Kuna tetesi Vinicius anafikiria kuondoka. Anaona zama zake Madrid zinakaribia mwisho. Mwenye mpini kwa sasa ni Alonso, akiamua ataondoka asipoamua hatoondoka.
Huwa inatokea, kuna wakati Zlatan Ibrahimovic aliwahi kusema ugomvi mkubwa kati yake na Pep Guardiola ilikuwa ni hataki awe mkubwa kuliko timu, alidiriki kumwambia hatakiwi hata kuendesha baadhi ya gari zake za thamani.
Mwishowe, mambo yaliharibika baina ya watu hao wawili na hata ikasababisha Ibra aondoke. Makocha wapya wanapoingia katika timu huwa lazima kuna wachezaji watapata faida na kuna wachezaji wataondoka.
Inawezekana mimi na wewe miezi sita nyuma kutoka sasa tusingeweza kuamini itafikia mahali Vinicius ataanzia benchi katika mechi ya michuano muhimu kama Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata alipoulizwa Alonso kuhusu kumweka benchi alisema anataka kila mchezaji apate nafasi, lakini Alonso huyu huyu haonekani akimfanyia hivi Kylian Mbappe.
Kocha mpya anapoingia katika timu huwa anahitaji wachezaji fulani kutokana na aina fulani ya mbinu zake na akiona humfai haijalishi ni staa kiasi gani atakuondoa tu na kuna muda mwingine huwa ni hulka tu ya mwanadamu ni ngumu sana kuelewa makocha wa mpira wa miguu.
Jose Mourinho alipokuwa anajiunga na Tottenham, Dele Alli alikuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo. Yeye na Harry Kane ndio walikuwa ni mastaa wa timu, lakini baada ya Mourinho kuingia, hilo ndio lilikuwa anguko la Dele, hadi leo ana tanga tanga.
Juan Mata aliondoka Chelsea kwa sababu ya Jose Mourinho na baada ya kocha huyo pia kutua Manchester United na kukutana naye hapo, mambo yakaendelea kuwa ni yale yale.
Kuna wakati Mourinho alimwingiza Mata kipindi chapili cha mechi na baada ya muda akamtoa. Jambo la ajabu kidogo, alipoulizwa akasema alimtoa kwa sababu Mata ndio alikuwa mchezaji mfupi kuliko yoyote.
Yaya Toure alipoondoka Barcelona kwenda Manchester City, moja ya sababu ilikuwa ni kutoelewana na Guardiola.
Tangu kuanza kwa msimu huu, ni mechi moja tu kati ya sita za La Liga ambazo staa huyu alicheza kwa dakika 90 lakini zilizobakia zote alicheza chini ya dakika 80.
Msimu uliopita katika mechi sita za mwanzo za La Liga za Madrid, mbili alicheza dakika 90 na zilizobakia zote alicheza dakika 80 na kuendelea.
Katika msimu uliopita, mechi zote za Ligi ya Mabingwa alizoanza, alicheza dakika zote 90, lakini msimu huu tayari ameshacheza mechi moja tu ambayo alitumkia kwa dakika 27.
Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na inaelezwa anataka mshahara sawa na ule ambao Kylian Mbappe analipwa lakini Madrid imemwambia haitomwongeza kufikia kiasi hicho, ni kama akitaka abaki asipotaka asibaki.
Maisha yameenda kasi sana kwa mshkaji wetu, utawala wa Alonsi umempa ladha nyingine ya ulimwengu wa soka. Mimi nawewe hatujui kinachotokea Kiwanjani, lakini huenda mtindo wa maisha wa wachezaji wa Amerika ya Kusini na Kaskazini ikawa sababu moja wapo inayomweka katika hali hii.
Tunajua washkaji ni watu wa bata sana, wanaamini mpira siku zote upo miguuni mwao, watacheza tena, hawahitaji kujitesa sana, inawezekana pia Alonso ameamua tu mwenyewe kama anavyosema, mwisho ukweli anaujua yeye, ila ndio hivyo kadri siku zinavyozidi kwenda gurudumu nalo linazidi kumwacha Vinicius.