Vinicius anawindwa kama swala England
Muktasari:
- Tangu kuanza kwa msimu huu, mara kadhaa Vinicius ameripotiwa kutaka kuondoka Madrid na hata alisikika akisema bora aondoke, jambo lililoziaminisha klabu hizo za England kuna nafasi ya kuipata huduma yake.
MANCHESTER United, Manchester City, Chelsea na Arsenal, zimeripotiwa kuwasiliana na wawakilishi wa mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior, 25, ili kuulizia uwezekano wa kuipata saini yake dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Tangu kuanza kwa msimu huu, mara kadhaa Vinicius ameripotiwa kutaka kuondoka Madrid na hata alisikika akisema bora aondoke, jambo lililoziaminisha klabu hizo za England kuna nafasi ya kuipata huduma yake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, sababu kubwa iliyokuwa inasababisha Vinicius ahitaji kuondoka ni kocha wa wakati huo Xabi Alonso ambaye hakuwa katika maelewano naye mazuri.
Alonso alikuwa akimwanzisha Vinicius benchi mara kadhaa na wakati mwingine alimfanyia mabadiliko ya mara kwa mara jambo lililokuwa likimkera sana Vinicus.
Hata hivo, kwa sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri kati ya Mbrazil huyu na benchi la ufundi la Madrid, lakini hiyo haijazipotezea matumaini timu nyingi za England ambazo zimeendelea kuwasiliana na wawakilishi wake.
Mohamed Salah
LIVERPOOL huenda ikabadilisha uamuzi wake wa kumwachia mshambuliaji wao wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na badala yake inaweza ikahitaji kupewa mshambuliaji wa Brazil, Marcos Leonardo, 22, anayekipiga Al Hilal kama sehemu ya ofa.
Salah, ambaye ni miongoni mwa wachezaji bora katika historia ya Liverpool, mwezi uliopita alitangaza ataondoka Liverpool ifikapo mwisho wa msimu huu.
Katika makubaliano ya awali licha ya kuwa bado ana mkataba unaomalizika mwakani, Liverpool ilikubali kumwacha aondoke kama mchezaji huru.
Manuel Ugarte
MANCHESTER United ipo tayari kumuachia kiungo wake, Manuel Ugarte, 24, dirisha la majira ya kiangazi, ikiwa itapata ofa nzuri. Kwa mujibu wa ripoti, timu kadhaa tayari zimeonyesha nia ya kumsajili, ikiwa pamoja na Newcastle United, Aston Villa. na Juventus. Ugarte kwa sasa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Man United hali inayochangia hata yeye kutamani kuondoka.
Amadou Onana
KIUNGO Aston Villa, Amadou Onana, 24, anahusishwa anaweza kuondoka katika klabu dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ripoti zinaeleza Manchester United ni miongoni mwa timu zinazomfukuzia ikiamini atasaidia kuimarisha zaidi safu yao ya kiungo.
Onana ambaye ni miongoni mwa mastaa tegemeo wa Villa, anasifika zaidi linapokuja suala la kusaka mipira pale timu inapopoteza umiliki.
Luka Vuskovic
BEKI wa Tottenham Hotspur, Luka Vuskovic, 19, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Hamburger SV, anatarajiwa kurejea katika klabu hiyo msimu ujao baada ya kiwango chake kuimarika sana akiwa huko Ujerumani.
Awali, uongozi wa Spurs ulikuwa unafikiria kumuuza staa huyu mazima lakini Vuskovic amezidi kuonyesha kiwango bora siku hadi siku kiasi cha kuwafanya vigogo hao wasitishe mpango wao wa kwanza. Licha ya kuonyesha nia ya kurudi Tottenham, beki huyo pia ana ofa kutoka kwa timu kadhaa barani Ulaya.
Robin Roefs
CHELSEA inaripotiwa kufikiria kutaka kumsajili kipa wa Sunderland, Robin Roefs, 23, ili akawe mbadala wa kipa wao wa sasa, Robert Sanchez ambaye amekuwa akifanya makosa ya mara kwa mara yanayoigharimu timu.
Roefs ni moja kati ya nguzo muhimu sana za Sunderland ambayo imekuwa katika mwenendo mzuri msimu huu licha yakuwa ndio imepanda daraja. Sanchez amekuwa akihusishwa kuondoka tangu mwaka jana, sababu kubwa ikitajwa ni benchi la ufundi kutokuwa na imani naye kwa sababu anafanya sana makosa.
Yan Diomande
BAYER 04 Leverkusen inaripotiwa kupanga kumwongeza mkataba wa muda mrefu zaidi mshambuliaji wake chipukizi, Yan Diomande, 19, baada ya kuona vigogo wengi barani Ulaya wameanza kuinyemelea huduma yake.
Diomande, ambaye anaichezea timu ya taifa ua Ivory Coast, amekuwa akiwindwa sana na timu kubwa za Ulaya tangu Januari kutokana na kiwango chake. Hivi karibuni maskauti wa timu kadhaa pia wameonekana katika mechi za Leverkusen wakiendelea kufuatilia maendeleo yake.
Maxence Lacroix
LIVERPOOL bado inaendelea kupigana vita kali na Bayern Munich ili kumsajili beki wa kimataifa wa Ufaransa, Maxence Lacroix, 25, anayekipiga katika kikosi cha Crystal Palace.
Inaelezwa, Bayern ipo tayari kutoa ofa nono zaidi ya ile ambayo Liverpool ilikuwa inajipanga kutoa hivyo kufanya mvutano uongezeke zaidi. Mkataba wa sasa wa Lacroix unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao matatu.