Vigogo wawili wazidi kumgombea Wirtz

Muktasari:
- Wirtz mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akihusishwa kwamba anaweza kuondoka mwisho wa msimu uliopita lakini aliamua kuendelea kubakia Leverkusen.
MANCHESTER City, Liverpool na Arsenal wanamnyatia kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini timu yake inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 103 milioni.
Wirtz mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akihusishwa kwamba anaweza kuondoka mwisho wa msimu uliopita lakini aliamua kuendelea kubakia Leverkusen.
Fundi huyu amekuwa akiwindwa na vigogo wengi barani Ulaya ambao walivutiwa sana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita ambapo aliisaidia timu yake kuchukua ubingwa wa Bundesliga.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 41 za michuano yote, amefunga mabao 15 na kutoa asisti 13.
Matheus Cunha
MANCHESTER United wametuma maombi kwenda Wolves kuomba kulipa ada ya uhamisho ya kumsajili kiungo Matheus Cunha kwa awamu katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu.
Staa huyu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, ana kipengele katika mkataba wake ambacho kinamruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 62.5 milioni. Mbali ya Man United, saini ya staa huyu pia inawindwa na Arsenal, Newcastle na Nottingham.
Diogo Costa
CHELSEA imeingia kwenye vita dhidi ya Manchester United na Manchester City ili kuipata saini ya kipa wa FC Porto, Diogo Costa, mwenye umri wa miaka 25.
Benchi la ufundi la Chelsea linamhitaji kipa huyu baada ya Roberto Sanchez kutoonyesha kiwango bora hivi karibuni. Man City pia inamhitaji ili kuziba pengo la kipa wao raia wa Brazil Ederson, mwenye umri wa miaka 31, ambaye yuko kwenye mazungumzo na timu za Saudi Arabia.
Mohammed Kudus
WINGA wa West Ham na timu ya taifa ya Ghana, Mohammed Kudus mwenye umri wa miaka 24, ameingia katika rada za Al-Nassr inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambayo ipo tayari kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kudus anaonekana kuwa ingizo sahihi kwenye safu ya ushambuliaji ya AL Nassr kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha tangu atue West Ham.
Raphinha
AL-Hilal ya Saudi Arabia imevutiwa na mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Raphinha, 28, ambaye msimu huu yupo katika kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu. Staa huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, amewekewa mezani ofa ya mshahara wa karibia Pauni 1 milioni kwa wiki. Msimu huu amecheza mechi 49 za michuano yote na kufunga mabao 30 na asisti 25.
Dean Huijsen
BEKI kisiki wa Bournemouth na timu ya taifa ya Hispania, Dean Huijsen, 20, ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na Real Madrid kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Dean amekuwa katika rada za vigogo wengi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu huu. Mkataba wake wa ssa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Marcus Rashford
TOTTENHAM wanapanga kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Rashford anahusishwa kuondoka katika dirisha hili ikiwa ni baada ya kukosana na kocha wake Ruben Amorim mwaka jana hali iliyosababisha atolewe kwa mkopo kwenda Aston Villa, Januari mwaka huu.
Kaua Santos
MANCHESTER United na Tottenham wamefanya mazungumzo na Eintracht Frankfurt kuhusu uwezekano wa kuipata saini ya kipa wa timu hiyo wa kimataifa wa Brazil, Kaua Santos ambaye anaweza kuuzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 30 milioni.
Santos mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.